Kila mtu anapenda watoto wachanga. Hata jitu ambalo huwa mara
nyingi halicheki na mtu liko siriaz wakati wote likikutana na katoto kachanga
utakuta linaanza kutabasamu, tena likikabeba katoto kachanga utaona nalo
linageuka kuwa litoto. Utaona linaanza kuongea na katoto kachanga lugha za
ajabu kabisa utadhani wanaelewana, utasikia, ‘Shum Babu toto shum babu, au shum
bibi, shum antii aijigijigijigi, awawawawa, abububujijiji’ na maneno mengine
yasiyoeleweka eti ndio mtoto atacheka. Leo niwape siri, mnajua kwanini vitoto
huwa vinacheka sana? Vitoto vichanga vimezaliwa na akili sana, sasa huwa
vinacheka kuona baba zima au mama zima halijui kuongea vizuri, kitoto
kinajisemea moyoni, ‘Huyu mkubwa mzima badala ya kuongea mambo ya maana eti
anasema abujibujibujibuji’ kimsingi watoto wachanga wanawacheka sana, muwe
mnaongea nao kikawaida, sawa ndugu zangu?
Leo niwape ushauri wababa wenzangu kuhusu
taratibu mbalimbali za kufwata kabala ya kucheza na watoto wachanga,
kama nilivyosema vitoto vichanga vina akili sana, hivyo basi sio
kuanza kuvibeba kabla ya kujitayarisha. Najua wabishi wameshakaa mkao wa
kubisha, lazima saa hizi wanasema kimoyomoyo,’ Hakuna kitu kama hicho, watoto
ni malaika’. Mi nasema sawa hebu nisikilizeni kwanza. Wababa wenzangu, sharti
la kwanza usicheze na mtoto mchanga ambaye ndio kwanza katoka kunyonya wakati
umevaa shati la au koti lako la bei mbaya, hakikisha imeshapita japo nusu saa
tangu amenyonya ndipo uanze kumrusharusha. Watoto hawa wajanja sana, wakijua
kuwa umevaa kitu cha bei mbaya watakutaim na kutumia nafasi hiyo
kukucheulia maziwa na kama hukujiangalia vizuri unaweza ukaingia kwenye
daladala na michirizi ya maziwa ya mgando mgongoni.
Sharti la pili linahusu wale ambao hupenda kucheza na watoto kwa
kuwanyanyua juu ya vichwa yao, kabla hujaanza kamchezo hako, hakikisha mtoto
kavaa nepi. Katoto kakijua una kamchezo hako, katajifanya kanacheka sana na
kufurahi kila ukikanyanyua juu, kumbe huo mtego, iko siku ukikanyanyua juu kama
hakana nepi katakutaimu na kukukuharishia kichwani, chunga sana, maana
inawezekana wakati huo mdomo wako uko wazi. Hutu tutoto twa siku hizi
tunaanzaga ukorofi tumboni.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE