Sisi
wenye vyombo vya usafiri baada ya kuvumilia kwa muda mrefu tumeona tutoe
dukuduku letu kuhusu nyinyi watembea kwa miguu wa Tanzania hususani nyinyi wa
Jiji la Dar aka Bongo. Watembea kwa miguu mnasababisha kero kwa siye wenye
vyombo vya usafiri. Yapo mengi mnayofanya lakini hapa kwa waraka huu wa kwanza tumeamua
kutaja machache.
i.
Kila mtu anajua taa zile zinazobadirika rangi kwenye njiapanda mbalimbali
zinaitwa, 'taa za kuongozea magari’, hivi kwa nini na nyie eti mkiona taa ya
kijani ina picha ya mtu mnaanza kuvuka barabara? Hamuoni mara ngapi
mnakoswakoswa na vibajaji na bodaboda? Hamruhusiwi kuvuka mpaka sisi tuwe
tumemaliza ishu zetu jamani, mnatuchanganya. Kazi ya zile taa zote pale barabarani ni kama
ifuatavyo, taa nyekundu maana yake dereva punguza mwendo kama hakuna gari jingine
endelea na ishu, pia hata ikiwaka kijani au njano kwa sisi madereva maana ya
hizo taa haibadiliki, sasa nyinyi kwanini mnakuwa kimbelembele? Au kwa kuwa ni
rangi ya chama basi mnajiona wajanjaa. Ok nategemea mmeelewa kuwa taa zile
haziwahusu ni za kuongozea magari si kuongozea watu.
iii.
Inaitwa kwa kizungu Zebra Crossing kwa Kiswahili alama za Pundamilia, kwanini nyie
mmeamua kuwa ni sehemu za kuvukia binadamu, yaani lets be honest inaudhi
sana. Mtu uko kwenye gari lako, umewasha AC, uko spidi 80, muziki mzito
unapiga, mkononi una Blackberry unatuma TXT, ghafla mtu anaamua kuvuka barabara
kwa kuwa kuna alama za pundamilia, huu ukorofi utakuwa umepangwa na wapinzani kuharibu taratibu tu hakuna sababu nyingine. Jamani hebu niwaeleze, alama zile ziko kwa
sababu kuu 2. Kwanza wataalamu wetu wameona kwenye sinema nyingi huko Ulaya, na wengine wamesoma huko,
hizo alama zinachorwa sehemu nyingi barabarani kwa hiyo ili barabara zetu zifanane na za
Ulaya ikaonekana ni vizuri na sisi tuwe na hizo alama. Pili barabara zikiwa
nyeusi tu kwa muda mrefu siyo vizuri kwa hiyo unaweka alama hizo za mabaka
meupe kuondoa monotony, kupamba barabara. Hata ulaya kwenyewe inajulikana alama hizo ni za Zebra
Crossing yaana mahala pundamilia huwa wanavukia barabara sasa niseme nini
zaidi?
Nashauri serikali itengeneze semina elekezi kule Ngurudoto ambapo
watembea miguu wote waende wahudhurie semina kwa siku mbili ili kujua ukomo wao katika
matumizi ya barabara.Mkuu wa wenye vyombo vya usafiri