13 December 2017
WATOTO WA SIKU HIZI WANAANZA MAISHA NA STRESS
Wakati wa utoto wetu ilikuwa raha sana, unaamka asubuhi unakuta chai au uji unakunywa tena kama hakuna andazi au mkate unalilia mpaka upatikane , ukisha kunywa unatoka nje kwenda kucheza na wenzio mpaka wakati ukiitwa kwa ajili ya chakula cha mchana. Hata usipoitwa njaa ikianza kuuma unarudi nyumbani na kudai chakula, kimetoka wapi, nani kapika hayakuhusu. Hakuna stress. Lakini siku hizi kuna wazazi wanawapa watoto wao stress mpaka unawashangaa. Kisingizio kikiwa eti ndio maendeleo. Hebu fikiria siku hizi watoto wanaosoma nasari nao wanapewa homwek, jamani muwe na huruma, mtoto akirudi toka shule badala ya kwenda kucheza na wenzie anajipinda kufanya homwek, waalimu na wazazi wanagangamala kabisa wanamwambia mtoto hakuna kucheza mpaka umalize homwek, na mtoto masikini anajipinda maana anajua asipomaliza atakuwa na adhabu shuleni kesho yake. Mtoto anaanza maisha na stress, tumeiga wapi sijui maana hata wazungu wenyewe walioanzisha nasari hawawapi watoto wao homwek. Mtoto anakuwa hajui hata namna ya kujichanganya na wenzie na ndio maisha yake yote anakuwa mtu wa aina hiyo. Utoto wetu kulikuwa na stress moja tu. Siku mama yako atakapoamua kukutuma gengeni utasikia ‘ We Joni, hebu nenda hapo gengeni kanunue mchicha, ukikuta wanauza fungu shilingi hamsini nunua, kama wanauza fungu shilingi mia usinunue, nunua matembele, lakini kama matembele wanauza fungu shilingi mia, basi nunua kisamvu cha shilingi hamsini, lakini kama kisamvu nacho wanauza shilingi mia , basi nunua mchicha wa mia’ Ukishapata maelezo hayo unakimbia haraka uwaho kurudi utimize amri uende kucheza, lakini ukifika gengeni umechanganyikiwa wala hukumbuki ni nini hasa ulitumwa, kama ni mchicha au matembele au kisamvu, hapo ndipo stress ya utoto inapoanza ukifikiria kitakachokukuta ukirudi na kuulizia upya, “Eti mama ulinituma nini?” Hizo ndizo stress za utoto. Na stress nyingine kubwa ilikuwa pale unaposhtuka asubuhi na kukuta umekojoa kitandani, hapo inalazimika ubaki kitandani , umejifunika na shuka gubigubi mawazo yote kwenye kipigo kinachokusubiri
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE