11 October 2012

HURUMA YANGU NI MUHIMU KWA MAISHA YAO

Kuwa na huruma sana inaponza sana, kwa mfano wa karibu ni mimi. Unajua mimi ni mtu mwenye huruma sana, na hii inanikosti. Lakini bahati mbaya hiyo ndio tabia yangu, siwezi kubadilika. Unajua kwa mfano isingekuwa huruma yangu ya hali ya juu leo hii ningekuwa sinywi pombe kabisaaaa unaonaee. Lakini mara nyingi nikiwa na glasi ya mwisho ambayo huwa najisemea baada ya glasi hii sinywi tena, utaona huruma yangu inaanza kunisuta. Maana naanza kufikiria ni watu wangapi ambao maisha yao yanategemea wanywaji kama mimi kuendelea kunywa? Kuna wakulima wa ngano ambao ikiwa wanywaji wote tutaacha kunywa na wao watakosa kipato cha kuuza mazao yao kwa watengeneza pombe, maisha ya watoto wao itakuwaje? Haya baada ya hapo kuna hizi kampuni za kutengeneza pombe, tena siku hizi ukienda kwenye makampuni makubwa kuna wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi, kaimu wakurugenzi, mameneja, wahasibu , wahudumu wa ofisi, madreva, wafanyakazi viwandani, watu wa masoko, wenye baa, wahudumu wa baa, yaani nikiwaza kuacha pombe naanza kufikiria watoto wa hawa watu wote wananitegemea mimi, halafu kitendo cha kufanya ukatili mkubwa wa kuwanyima haki yao ya kuishi kwa ajili ya ubinafsi wangu tu kinanisuta sana? Tena siku hizi unakuta mpaka wasanii toka nje wanatakiwa kuja kuponea fedha zangu ili watoto wao waende shule, kwa kweli huruma yangu naona ni muhimu kuliko ubinafsi wangu. na hapo ndipo huwa naagiza nne mfululizo, sio kwa sababu napenda pombe jamani ni huruma kwa hawa wote ambao maisha yao hapa mjini yananitegemea umeonaee. Tujitahidi jamani ili kusaidia wenzetu

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE