Yaani baba
mkwe katoa mpya juzi, mpaka sasa bado sijajua nicheke au nisikitike, maana
nasema tena baba mkwe katoa mpya. Juzi Jumamosi tulifanikisha sherehe ya harusi
ya mtoto wa kiume wa rafiki yetu. Sisi ndio tulikuwa wanakamati hivyo kwanza
nijisifu tuliwezesha bonge ya harusi, japo huwa nawaza tu ule mkwanja
tuliokusanya wangepewa hawa maharusi hakika wangemaliza umasikini na kuanza
maisha ya kifahari, lakini ndio hivyo tena tulipanga kutumia mamilioni yote
yale kwa ajili ya kula na kunywa kwa masaa machache tu.
Turudi kwa
baba mkwe, sherehe ilianza vizuri kabisa, MC alikuwa mmoja wa wale ma MC ambao
wanapenda kusikia sauti zao wenyewe basi anaongea huyo, kila jambo analirefusha
mpaka inachosha. Hatimae ikafika wakati MC akatutangazia kuwa baba mkwe anataka
kuja kutoa wosia. Binafsi kipengele hiki huwa kinanichekesha sana, kama mtoto
hakupewa malezi mazuri, haka kahotuba ka dakika za mwisho ndio kweli
katarekibisha tabia zao kweli? Tuache hayo, baba mkwe akakamata maik, akasalimu
‘Mambo?’. Hapohapo nikashtuka, nikaona baba mkwe huyu wa kileo sana, baada ya
kumcheki vizuri nikagundua kuwa kinywaji alichokuwa amekunywa vimemchangamsha
kidogo. Baba mkwe baada ya kujibiwa salamu zake akaanza hotuba ambayo
sitaisahau mapema. ‘Kijana upo? Naona umeamua kumuoa binti yangu, mimi kama
baba yake nasema wazi inaonekana humfahamu binti yangu vizuri, mtu anaemfahamu
binti yangu hawezi kufanya uwenda wazimu wa kutaka kumuoa huyu mtoto’. Dahh
ukumbi mzima ugeuka kimyaa, bibi harusi alikuwa kajiinamia. ‘Huyu binti yangu
ni mkorofi katusumbua sana mimi na mama yake, toka alipofikisha umri wa miaka
kumi na sita. Kafukuzwa shule tatu, kila shule ikilalamika kuwa anawaharibu
wanafunzi wenzie. Hatimae shule ikamshinda, kifupi sijui haswa baada ya hapo alikuwa
anaishi wapi. Japo mara chache alikuwa analala nyumbani. Huyu binti yangu hebu
fikiria hata instagram walifungia ukurasa wake kutokana na picha alizokuwa
akiziweka humo. Nadhani kijana ulimuona picha zake kwenye magazeti ukaona
umepata malaika, hafai kabisa huyo hafai. Nimeona nikueleze ukweli usije baadae
kunilalamikia mashetani yake yakimpanda. Mimi na mama yake sasa tunaondoka,
tulikuja kuwaonya tu ili msije kutusumbua baadae, pole kijana wangu’ Baba mkwe,
mama mkwe, mashangazi, wajomba, makaka haooo wakasepa.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE