Unajua kila zama zina mambo yake , teknolojia nayo
inasababaisha kuweko mambo ambayo wazee kama mimi tunabaki kushangaa tu nini
kinaendelea. Katika jambo ambalo limefanya mabadiliko makubwa ni eneo la
sherehe za harusi. Enzi zetu watu walikuwa wanatafutiwa wachumba, mwanaume
unaambiwa kuna binti umetafutiwa lazima ukubali, na mabinti vile vile
wanatafutiwa mume na hakuna kubisha, taratibu zote zinafaywa na wazee wewe
unakabidhiwa mzigo tu.
Siku hizi ndugu yangu kila harusi inatengeneza vipengele
vipya. Zamani bibi harusi na bwana harusi walikuwa ni watazamaji tu wa sherehe
yao wenyewe, siku hizi wanashiriki kila kitu ikiwemo kutoa hotuba. Wiki
iliyopita niliingia kwenye harusi ambayo bwana harusi alitoa hotuba kali sana.
Baada ya MC kututanganzia kuwa bwana harusi ana machache ya kusema tukaanza kumsikiliza. Akiwa na suti yake
maridadi akakohoa kidogo kasha akaanza, ’Asante MC, kwanza naomba nimshukuru
Mungu kwa kumuumba mke wangu, kwa hilo Mungu uko juu. Pili nimshukuru baba
mwenye nyumba wangu kwa kukubali niwe na deni la kodi ili kufanikisha harusi
hii. Naomba nitoe shukrani kwa bosi wangu kwa kunipa likizo fupi ili
nikamilishe shughuli hii. Naishukuru kamati yangu ya harusi kwa kuwezesha
kukusanya fedha zilizofanikisha kulipa mahari, nimshukuru mke wa kaka yangu kwa
kutuazima gauni la harusi, na kaka yangu kwa kuniazima suti hii niliyovaa.
Natoa shukrani kwa mtengeneza keki, leo hakuna kukata keki, nitairudisha keki
kwako kesho kama tulivyokubaliana. Nawashukuru wazazi wangu kwa kuja na kikundi
cha ngoma toka kijijini, kweli kimeziba pengo la burudani katika harusi hii.
Naishukuru kamati ya wazee wa kanisa kwa kufanikisha kumshawishi mke wangu
aolewe na mimi, niwape aksante kwa akina mama jirani kwa kuja na vyakula toka
makwao ili kufanikisha harusi hii, na vijana kwa kuja na pombe za halali na
haramu mradi harusi hii ni furaha tupu. MC wewe ni rafiki yangu nashukuru kwa
kukubali tulipane kidogokidogo aksante sana’ Kisha bwana harusi akakaa chini
watu wote tukabaki kimyaaaaa
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE