Mi nadhani hizi
taratibu za zama zenu hizi za kuruhusu hotuba kutolewa kwenye sherehe za
harusi zingeangaliwa upya, turudi kwenye taratibu safi za enzi zetu, ambapo hakukuwa
na mambo ya hotuba, mara ya bibi harusi halafu ya bwana harusi, halafu hotuba za wazazi, siku hizi na wenyeviti wa
kamati nao wanaongea, basi vurugu tupu. Au la, hotuba zihakikiwe, mtu atakae
taka kuongea aandike kabisa hotuba yake na kuituma kwenye kamati ya harusi ili ihakikiwe. Nasema hivi kwa kuwa Jumamosi
iliyopita nilihudhuria sherehe za harusi kwenye ukumbi wa mji mmoja unaojisifu
kwa kuwa ndio chanzo cha mapenzi, baada ya shamra shamra za kila aina
zilizokuwa zinaendeshwa na MC mdada mmoja mwenye jina matata sana.
Tukatangaziwa kuwa baba mzazi wa kijana
ana machache ya kusema na kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa, baba hakusema sana
zaidi ya kumtakia mwanae maisha mema yenye raha. Kisha tukatanganziwa kuwa mama
wa bibi harusi anataka kuongea,hapo ndipo vituko vikaanza. Mama mkwe
alisindikizwa na akina mama wenzie ambao walikuwa wamevalia Madera mekundu
sare, wimbo wa Msagasumu uliporomoshwa,
mama mkwe na kundi lake wakaanza kumwaga razi kwa mauno ya nguvu, nikamuangalia
bibi harusi nikakuta anashabikia kwa kupiga makofi na kufurahi alikuwa kama nae
anataka kwenda kujiunga na mama yake, wakati bwana harusi alionekana kushangaa
vituko vya mzazi wake mpya. Hatimae mama harusi akapewa maik, hapohapo akaanza,
‘Halo halo ya harusiii’ watu wote tukajibu ‘Haloooo’. Mama mkwe akakaa sawa na
kuanza kutoa nasaha. ‘ Mwanangu hongera kwa kuolewa, walisema sana mtaani,
naona umewaziba midomo wale mashoga zako wasiojua kuoga haloooo. Haya baba, mke
ndio huyoo umepata, mwanangu mzuri kama unavyoona, hana kovu mwanangu, labda
kama hizo tatuu zake za mgongoni na tumboni utaziita makovu. Mwanangu kalelewa
kwa uhuru anapenda starehe, na wewe mlikutana disko nisisikie unaanza kumbana
eti asiende disco, mwanangu anapenda ngoma na nimemlea apende utamaduni wake,
sasa nisisisikie eti ohh unamfungia ndani asiende kupandisha mzuka ngomani,
mwanangu sio dobi, nguo zako peleka kwa dobi, mwanangu sio mpishi wa hotelini
hivyo sio kumlazimisha apike akaja ungua
na miuji ya ugali bure hana kovu huyo. Mwanangu kifupi ukiona yanakuzidi, rudi
kitanda chako ziuzi wala sigawi, wanaume nawajua mie. Haloooo’
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE