Hahahahaha
yaani kila siku Bongo kuna kichekesho kipya, mi nashangaa unamkuta mtu kanuna
siku nzima anapata mastresi na pengine kupata vidonda vya tumbo na presha
wakati mambo ya kuondoa presha yamejaa kila kona. Hebu angalia kwa mfano jinsi
Wabongo walivyo mabingwa wa visingizio, kila jambo likikwama kuna bonge ya
kisingizio. Kwa mfano ukishamlipa mganga wako wa kienyeji mihela kibao ili
akuunge na Frimason ili wakupe dawa ya utajiri, unajikuta siku zinapita hakuna
cha utajiri wala nini, ukienda kwa mganga wako kumuuliza ndipo atakapoanza
visingizo, kwanza anaanza kukuuliza, ‘Ulifwata masharti yote niliyokwambia?,
Uliweza kutoa sadaka ya siafu kumi wa kiume?’ Ukisita tu kujibu, ndipo ataanza,
‘Unaona hilo ndio tatizo lenu nyie wateja, sisi tunaongea na mizimu inatoa
masharti nyie hamfuati halafu mnalalamika’ Hapo hata ujitetee kuwa hakukwambia
hilo atang’ang’ania kuwa alikutaarifu wakati anakupa ile dawa ya kinga ya
kuzuia wabaya wasikuone utakapotajirika. Juzi niliingia kwenye ofisi za kampuni
moja ya simu kulalamika kwanini kila nikinunua bando ya siku inaisha kabla siku
haijaisha, nikinunua bando ya wiki inaisha baada ya siku tatu. Dahh kabinti
flani emeizing kalikokuwa kanaongea Kiswahili cha mahauzgelo wa wazungu, kakaniuliza
jina, umri, kazi ninayofanya, idadi ya watoto, kisha kuomba kuona aina ya simu
ninayotumia. Halafu ndo kakaanza kuleta kisingizio. “Mzee umeshasoma masharti
yetu kuhusu bando?” Nikakaambia sijawahi kuyaona kwani yako wapi? ‘Sasa mzee we
unatumia bando zetu bila kujua masharti yake? Wewe kama mteja unatakiwa ujue
masharti yetu. Sisi kama kampuni tunakata vati kwenye hela yako ya bando, pia tunakadiria
masaa ambayo yako katika mzunguko wa eataim yetu na kulinganisha na thamani ya
dola ya siku hiyo, ndio tunajua siku hiyo ina masaa mangapi nadhani umeelewa ?” Sikuwa
nimeelewa nikaondoka taratibu bila kuaga. Ila kali zaidi ni ya huyu jamaa yangu
aliyetembelewa na mkewe ghafla
ofisini kwake, akakutwa kampakata sekretari wake wananyweshana chai, mama wa
watu alipowaona moyo ukataka kumtoka, akili ikasimama kufanya kazi, muda
uliotosha kabisa kwa sekretari kutimua mbio na kumpita yule mama akiwa kasimama
mlangoni kama sanamu. Bosi akaanza kumkaribisha mkewe kama vile hakuna cha
ajabu kimetokea. ‘Aise wife karibu sikujua unakuja, yaani hapa kwa kweli
tunafanya kazi kwa stress sana, yaani serikali imebana matumizi mpaka inakera,
hebu ona wafanyakazi wawili tunalazimika kutumia kiti kimoja na kikombe kimoja
cha chai, hii haikubaliki kabisa yaani mi naona heri niache kazi nirudi kwetu
nikalime”
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE