Mikasa
mingine huwa ukisimuliwa unacheka badala ya kumuonea huruma aliyekumbwa na
mkasa huo. Jamaa yangu mmoja huko Tanga juzi alivunjika mguu akakimbizwa
hospitali na wasamaria wema. Akapokelewa vizuri, daktaria akamuuliza jamaa
yangu kimetokea nini mpaka akavunjika mguu. Kwa mshangao wa daktari jamaa
akaanza, ‘Dokta mkasa huu ulianza miaka kumi iliyopita’ Dokta akashangaa,
akamwambia jamaa yangu sitaki
kujua yaliyopita nataka kujua imekuwaje ukavunjika mguu?’ Jamaa yangu
akasisitiza ‘ Dokta nisikilize kwanza nikuhadithie mkasa mzima sasa. Miaka kumi
iliyopita nilikuwa nafanya kazi ya upishi kwa bosi moja kule Ngamiani. Yule
mzee alikuwa na watoto watatu mmoja msichana. Huyu binti alikuwa mzuri sana,
vijana wote mtaani walikuwa wakijaribu kupata nafasi katika roho yake lakini
haikuwa rahisi kwa kuwa alikuwa akichungwa sana na baba yake na kaka zake. Mimi
sikuwa na tatizo lolote maana tulikuwa tukishinda nae pale nyumbani masaa mengi,
akinisaidia katika shughuli mbalimbali za mapishi jikoni. Kila mara jioni alikuwa
anakuja chumbani kwangu tunaongea mengi, na kila mara kabla hajatoka chumbani
kwangu alikuwa akiniuliza kama nahitaji kitu chochote, nilikuwa namjibu sikuwa
nahitaji kitu. Na kila baada ya jibu hili, alikuwa akicheka sana na kuondoka
zake. Kwa kweli nilikuwa nina uhuru wa mkubwa ndani ya nyumba ile, na mshahara
wangu ulikuwa mzuri sana, hivyo sikuona kama kuna kitu zaidi nilikuwa nahitaji.
Na hili liliendelea miezi mingi. Nikiri kwa kweli nilikuwa na mimi nampenda
sana binti huyu wa Kitanga, lakini nilikuwa naogopa kumtamkia hili, tuliendelea
kuishi hivi mpaka siku baba yake alipompeleka nje ya nchi kusoma, roho iliuma
sana kumkosa. Sasa dokta leo nilikuwa nimekwea mnazi nikiwa juu si ndio
kumbukumbu ikanijia kuhusu yule binti, na lile swali alilokuwa akiniuliza kila
alipomaliza mazungumzo ndipo akili
iliponijia kuwa lile swali kumbe mimi nilikuwa mjinga sikuwa nimemuelewa binti
yule miaka ile, alichokuwa anataka kunipa kumbe ndicho nilikuwa nakiota siku
zote, kwa bahati mbaya nikajisahau na kuachia mikono na kuanguka na kuvunjika
mguu’.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE