Aise
yaani huwezi amini ni kizungumkuti. Lakini swali kubwa ni hela kashika nani?
Maana kila mtu anasema hana hela sasa zimekwenda wapi? Juu ya hapo unasikia na
benki nazo zinalalamika kuwa biashara mbaya, sasa hela ziko wapi? Au wenye hela
wamezificha uvunguni mwa vitanda
badala ya kuzipeleka benki? Yaani
sielewi. Juzi baba mwenye nyumba kanifwata asubuhi kabla hata hakujakucha akanambia
hataki maneno mengi anataka kodi yake. Akili ikawa inanizunguka, mfukoni senti tano sina. Nilikuwa na
kativi kangu chogo nikaona nikaona bora nitafute mteja nikauze ili nipate japo
hela ya kumpunguza makali ya baba mwenye nyumba. Katika kutafuta wateja fundi tivi mtaani kwangu akanambia
kuna mteja alikuja kuulizia tivii ya bei rahisi hivyo kama ninayo yeye anaweza
kuiuza chapchap. Nikabeba mgongoni mali na kuipeleka kwa fundi, kisha
nikaelekea kuendelea na shughuli zangu. Kila dakika kumi nilikuwa nambip fundi
kujua nini kinaendelea. Hatimaye fundi akanambia biashara inaonekana imetiki,
mteja kaipenda mali yangu, kaahidi kuja kuichukua. Nilijisikia mzigo mzito
ukishuka kutoka mabegani kwangu, maana ningemlipa baba mwenye nyumba japo kidogo,
ningepata nafuu ya miezi kama mitatu hivi nijipange upya. Niliporudi nyumbani
nikamkuta baba mwenye nyumba ananisubiri, kakunja uso akionyesha hataki utani.
Bila kupoteza muda akanambia anataka hela yake leo leo. Nikatumia kila lugha
kumtarifu kuwa kuwa dili nafanya na kesho yake ningelipwa. Baada ya matusi ya
kutosha akaondoka na kunambia kesho yake anarudi acute pesa. Nikampigia fundi
kuulizia kuhusu mteja, fundi akanambia mteja akasema kuna mahala atalipwa hivyo
atachukua mzigo kesho yake. Mapema asubuhi nikatumiwa mesej na baba mwenye
nyumba, kuwa nitimize ahadi au patawaka moto. Nami nikamtumia fundi ujumbe
ajaribu kumkumbusha mteja ili alipe mapema. Kufikia mchana ngoma ikawa
palepale, mali yangu haijalipiwa na mteja aalikuwa kasema anasubiri pesa.
Wakati nawaza ntafanyaje mteja asipolipa, fundi akanipigia simu niende kwake
nikutane na mteja uso kwa uso tukubaliane. Nikaenda haraka kwa fundi huku
nasali kimoyomoyo kuwa mteja alipe japo kitu cha kumuonyesha baba mwenye
nyumba. Nilipofika kwa fundi si nikamkuta baba mwenye nyumba kumbe ndie mteja
wa tivi yangu. Nilijisikia miguu ikiishiwa nguvu
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE