16 November 2016

TILAMBU HOYEEEE


Haya tena kumekucha wengine wanasherehekea, wengine wanalia Trump ndio kishakuwa Rais wa Marekani. Huwezi kuamini kule kijijini kwetu kuna sherehe kubwa sana. Wanakijiji wanasherehekea Trump kuwa Rais. Najua utashangaa, hata mimi mwanzo nilishangaa, lakini ngoja nikupe mkasa mzima ujue sababu ya watu kucheza ngoma kusherehekea ushindi wa Trump. Nilikuwa nimeshachoshwa na kelele za mjini nikaona nirudi kijijini kama wiki hivi nikapumzishe akili. Kijiji chetu kiko kama kilomita 15 toka barabara ya lami hivyo ukishuka kwenye basi unaweza aidha kukanyaga kwa miguu au kupanda bodaboda. Nikachukua bodaboda, japo hunikuti nikipanda hiyo kitu hapa mjini, bodaboda za mjini zinatisha bwana, hawa jamaa udereva wao una uchizi ndani yake. Basi ile kukaribia kijijini tu nikaanza kusikia ngoma, baadae nikaanza kuona nyumba zimepambwa, niliposhuka kwetu namuona mjomba wangu mmoja yuko tilatila akanikaribisha, ‘Wamjini kalibu ufulahie maisha’.  Nikamsalimu na ndugu zangu wengine wote walionekana kuwa na furaha kubwa. Ndipo nikauliza kulikoni furaha zote au walikuwa wanajua nitakuja? Shangazi yangu moja akajitokeza na kupiga kigelegele cha nguvu na kusherehekea, ‘Tlambu Tlambu Tlambu hoyee’ Sasa wakanichanganya, Trump na kijiji chetu wapi na wapi? Waswahili dunia nzima wanahofu na ujio wa Trump hapa kwetu watu wanasherehekea, kuna nini?. ‘Shangazi Trump kafanya nini?’ shangazi akaniambia kikwetu ‘Hujasikia? Tlambu kashinda uchaguzi’. Nikamwambia nimesikia ila sijui kwanini wanafurahia. Shangazi akanikaribisha kwenye kiti akanambia,’Unamkumbuka yule binamu yako aliendaga Ulaya zamani?’ Nikamwambia ndio, kwani nani pale kijijini hamkumbuki yule mjinga, aliondoka zamani, kuna siku alirudi ila alifanya vituko vya mwaka, kwanza alijidai kasahau kikwetu , hata Kiswahili alikuwa anapata shida kuongea, pili alikashifu sana kijiji, na wanakijiji kuwa wachafu hawana maendeleo, na aligoma hata kuingia kwao akisema anaweza kupata maambukizi. Alipoondoka aliaacha simulizi ya muda mrefu kijijini. Nikamuuliza shangazi ‘Sasa kafanyaje yule kichaa?’ Shangazi akanambia, ‘Si unajua Tlambu kasema anawafukuza wageni wote Marekani? Basi binamu yako kanipigia simu juzi, anataka kurudi anaomba nimkatie kasehemu ka shamba tena kaongea kilugha vizuri. Sasa hapa tunamsubiri tuone ataingilia mlango gani hapa nyumbani Tlambu oyeee’,

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE