3 March 2017

MJINI NI SHIDAAA MAMBO SHAGHALA BAGHALA


Juzi niliamua kuzunguka mjini kuangalia vituko vya maendeleo. Yaani we acha tu, ushishangae kuona fenesi zimefungwa kwenye glasi za juis, wala usishangae kuona chandarua kimegeuzwa neti ya kuvulia samaki, mambo yako shaghala baghala. Lakini vituko vikubwa nilivikuta nilipoingia supa maketi. Baada ya kuchunguza kwa makini nikagundua kuna kitu cha ajabu sana kinaendelea, kumbe sio kila anaeingia supamaketi anaingia kununua kitu, watu wana sababu mbalimbali. Aina ya kwanza ya wateja ni wale wanaoingia kujipiga picha, wenyewe wanaziita selfie, yaana hawa wako kibao kila kona unakuta mtu anajipiga picha aonekane alikuwa supamaketi na haraka kuposti watsap na insta. Katika hili wadada ndio wengi zaidi ingawaje na kwa upande wa wakaka, wako wale wanaovalia suruali nusu mlingoti ndio idadi kubwa zaidi. Sasa hawa wakimaliza kujiselfisha mara nyingi hawanunui chochote ila wakijitahidi sana hununua bigi ji au maji madogo.

Halafu hapohapo wako madenti ambao wanapendana, basi hupanga kukutana supamaketi, hawa utawaona wanazunguka tu humo ndani hawatoki, wanajipiga selfi kibao ingawaje hawazipost insta, halafu mwisho hawanunui kitu. Mapenzi ya shule ni sheeeda. Kuna kundi la wateja ambao huingia supamaketi na kununua vitu ambavyo hata kwenye genge mtaani kwao vipo, lakini kwa kuwa supamaketi unapewa  mfuko una jina la supamaketi, hii ni swaga kubwa  mtaani, kila mtu anajua uliingia supamaket. Hawa huishia kununua mkate, au chumvi, wakijitahidi wataongeza na blubendi. Halafu kuna kundi la wamama washua, hawa huingia supamaketi na kikaratasi kimeandikwa kila kitu wanachotaka kununua, bahili hao, utakuta wanatembea na kalkuleta, wanaenda hesabu sambamba na mhudumu, mara nyingi hawa huja na watoto wao wakorofi, wanakimbia kimbia hovyo supamaketi, na ni wazi wanasoma intanesho, maana utasikia wamama hao kila dakika wakiita ‘ Junia, junia kam hia, Juni no stop that’ Wazungu weusi flani hivi. Halafu kuna wale wachunguza bei. Hawa huwa hawanunui chochote kazi yao kuzunguka tu supamaketi wanaangalia bei ya vitu, wanashika shika tu. Mara yuko kwenye sabuni, kahamia kwenye chakula mara aangalie sahani arudi kwenye sabwufa, akitoka hapo anaenda kwenye friza hawachoki hawa anaweza ingia supamaketi tatu kwa siku halafu hanunui kitu. Nitafute instagram @johnkitime nikuhadithie kitu

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE