Unajua kuna mama
ntilie mmoja pale mitaa ya Kijitonyama lazima sasa niongelee ishu zake. Mdada
huyu mpishi mkali sana, wali maji, wali nazi, pilau, biriani, uji wa mchele
vyote hivyo ukitaka utapata, bila kusahau ugali wa muhogo, ugali wa sembe
halafu alivyo na utaalamu ndie peke yake mjini hapa anaeweza kupika ugali wa ngano,
najua wabishi mtaanza ohh toka lini kukaweko na ugali wa ngano? Nyie nendeni
pale Kijitonyama.
Achana na ugali wa ngano, huyu mdada ishu kubwa kuliko yote
ni pilipili yake. Jamani kama duniani kuna kiungo kinachoweza kuleta apetait sana, yaani kinaweza kukufanya
uwe na hamu ya kula chakula kingi zaidi, kiungo hicho kinaitwa pilipili. Huyu
mdada wa Kijitonyama anatengeneza mwenyewe pilipili yake, sijui anatengenezaje
pilipili hiyo maana nilishakutana na pilipili kali lakini huyu mdada pilipili yake ni zaidi kali. Ukitaka kutumia pilipili yake lazima
ujitayarishe kisaikolojia. Ukijitia kukumia bila matayarisho unaweza kutamani
kukata ulimi laiv. Yalinikuta juzi nikaagiza biriani nikawekewa na pilipili
pembeni , haraka nikasambaza pilipili kwenye biriani yote. Nikachota kijiko kikubwa
kilichojaa biriani nikaweka mdomoni, ilichukua kama sekunde ishirini kwa akili
kupata habari kuwa kwenye ulimi kuna moto unawaka. Bila kuanza kudadisi, akili
ikatoa amri fasta kuwa lazima kutema hiyo biriani . Kulikuwa na jamaa mwingine
jirani yangu ambaye naomba nichukue nafasi hii kumuomba radhi kwani nilimuogesha
ile biriani kutoka mdomoni. Nilijaribu kuangalia maji yaliyokuweko jirani
ninywe nipunguze moto mdomoni, jicho
liliangukia kwenye maji ambayo muda mchache uliopita wateja tulinawa, hilo
halikunisumbua, haraka sana niliyagugumia, lakini wapi ulimi uliendelea kuwaka
moto, machozi yalikuwa yanatiririka bila aibu, nikakimbilia bomba la maji jirani
kulifungua hakikutoka kitu, kumbe maji yalishakatwa siku nyingi, ikabidi ninywe
tu maji waliyotumia kuosha viazi yaliyokuwa kwenye ndoo moja ya plastiki.
Kiukweli sitasahau maana nilitimka kukimbilia duka la jirani nikanunua soda
mbili baada ya kumaliza ndipo kidogo nikaanza kuona nafuu, akili ikaanza
kurudi. Pilipili ile huwa inanijia mpaka kwenye ndoto, kuna siku nikaota
nimeila tena nilizinduka usingizini na kukimbilia maji.
Kwa nini hukuita kikosi cha zimamoto?
ReplyDelete