Jana
nimepita nacheka kwenye mitaa ya kwetu, watu wengine wakawa wananiangalia kwa jicho
la kujiuliza, najua walikuwa wakidhani nimevuta moshi wa kitu kilichopigwa
marufuku, najua wengine watakuwa walikuwa wananionea huruma wakijua kuwa akili
yangu imepata msukosuko kidogo. Mi sikujali niliendelea kujipa raha mwenyewe na
kucheka zaidi. Mkasa niliokuwa nimeuona hata wewe ungekuweko ungecheka wiki
nzima. Nilikuwa nimekatisha kwenye
uchochoro mmoja ili niwahi kufika nyumbani, si unajua sie Wabongo kwa
vichochoro ndio wenyewe, mambo ya kufuata barabara kama magari sie hatuwezi
kabisa. Basi nikakatisha kichochoro kimoja, huko nikakuta kuna kelele ugomvi
mkubwa unaendelea, watu walishaanza kukusanyika, kama kawaida ya Mbongo yoyote,
lazima kujionea mweyewe kila tukio mubashara, nikajipenyeza kuona kulikoni.
Lohh hapo ndipo nilipoanzia kucheka, jamaa mmoja alikuwa kamkunja mwenzie ambae
kavaa mavazi maarufu kuvaliwa na Wamasai, sasa kwa vile kakunjwa shuka na kwa
vile hakua na vazi jingine, nusu ya mwili ulikuwa hadharani. Huyu mkunjaji kwa
lafudhi lazima alikuwa ametokea maeneo ya Kanda ya Ziwa, alikuwa anadai hela
yake. Inaonekana kuna siku hawa wawili walikutana sehemu, Mmasai akiwa anauza
dawa mbalimbali za kiasili, jamaa yangu kutoka Kanda ya Ziwa akaulizia kama
Masai ana dawa ya mapenzi akaambia ipo na inasemekana bei ilikuwa shilingi
arobaini elfu. Jamaa wa poti akazitoa na kurudi na dawa nyumbani kwa furaha
kubwa akijua kuwa yule kimwana wa Kizaramo aliyekuwa akimtamani siku nyingi
dawa yake imeshapatikana. Tatizo kubwa lilitokea siku alipofuata masharti yote
na kisha kuelekea kwa kimwana ambae alikuwa chaguo la moyo wake. Alipofika
akaanza kufuata masharti ya mwisho ambayo yalihusu kuzunguka nyumba ya kimwana
na kisha kuchota mchanga kidogo na kuweka mfukoni na hapo ni kumfuata kimwana
na kumgonga bega, mambo yote mazuri yangeanzia hapo, eti kimwana
angemkumbatia na kuanzia hapo kuwa
mali za Wapoti. Tatizo ni kuwa baada ya kufuata masharti yote ya Masai, Poti akaishia
kutandikwa makofi na kumwagiwa maji ya ukoko wa ugali wa ulezi na yule kimwana
na pia kutishiwa kupelekwa polisi. Kuanzia siku hiyo wa Poti alikuwa akimtafuta Mmasai ili
kurudishiwa pesa yake, sasa jana wamekutana. Palikuwa patamu hapo …..instagram@johnkitime
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE