22 March 2017

KUMBE SISI MABOSI FEKI



Marekani wamempata Rais, hata siku mia haja timiza, lakini hakika dunia nzima tunamsikia kwa mambo yake, mwenyewe anapenda mtandao wa twita huyo, haoni tabu kumkandia mtu kwenye twita. Sio mara moja anaviita vyombo vya habari, kuwa mabingwa wa taarifa feki.  Watu wote tulikuwa tunaamini kila kinachotangazwa na vyombo vya Marekani sasa tumezinduliwa, Rais wao mwenyewe anaviita feki. Nimekaa hapa nikawa nawaza nikaona na sisi huku kwetu kuna vitu kama vina harufu ya ufekifeki hivi. Yaani nimekaa nawaza hawa watu wanaoitwa na mara nyingine wao wenyewe wanajiita , watumishi wa umma. Unajua ukiwa mtumishi ina maana unamtumikia bosi wako, kwa hiyo mtumishi wa umma , bosi wake ni umma si ndio? Ina maana mimi na wewe ni mabosi wa hawa watumishi wa umma si ndio? Sasa mbona mambo yako kinyume? Wao mbona wanaekti kibosi na kutufanya sisi umma ndio vidampa, au ndio kusema sisi mabosi feki? Au sio?. Juzi nimeenda ofisi moja ya umma, nikawa naenda kwa mikogo nikijua mi ndio bosi nikataka kumuona mtumishi wa umma mmoja. Kufika pale nikaambiwa nimsubiri anahudumia wengine, poa nikakaa nje ya ofisi ya umma ambako kuna kaukuta kamejengwa kama benchi hivi, watu wengine watatu wakaniunga mkono. Akaja mtumishi wa umma moja ambaye ni mlinzi wa pale, akaanza, ‘Kwanini mnakaa hapo? Hebu tokeni hapo” Tukamuuliza “Sasa tukakae wapi?” Tukijua jamaa anajua sisi ndio mabosi wake. Akatujibu “Mie sijui ila tokeni mkakae hata kule barabarani”, nikajiona mi bosi feki kweli, huyu mtumishi wa umma anatufukuza umma, yaani anafukuza  mabosi wake?
Halafu hawa watumishi wetu  wanajua kuna watu wengi huwa wanakuja kutaka huduma na wanahitaji mahala pa kukaa, hawatengenezi mahala pa kukaa sisi mabosi wanaishia kutufukuza. Tena usije ukakosea ukakaa karibu na kituo cha polisi,  utatimuliwa ushangae mwenyewe, ole wako uulize, “Afande sasa nikakae wapi? Utaishia nyuma ya kaunta, na sio ya baa.

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE