Nakwambia
siku hizi hakuna kitu, stori tu nyiingiii lakini vitendo hafifu. Madoido ndio
mengii. Unajua zamani kabla wengi wenu hamjazaliwa watu tulikuwa sio wa mchezo
mchezo. Mdogo akimkuta mkubwa anamwamkia Shikamoo, sio huu mchezo wenu eti
mtoto mdogo anamwambia mkubwa ‘Heshima yako’, salamu gani hiyo? Yaani hivi
mnaona aibu kuamkia ‘Shikamoo’? Enzi zile kabla hamjazaliwa mtoto alikuwa
anamheshimu mkubwa yoyote yule, kma unamjua au humjui ukikosa adabu utakula
mikwaju barabarani toka kwa mtu hata humjui wala yeye hakujui, na ukirudi kwenu
husemi maana unaweza kuongezwa mikwaju. Watoto walikuwa wanaheshimu wakubwa,
hakuna maswali wala demokrasia kuhusu hilo. Enzi hizo kabla wengi wenu
hamjazaliwa kulikuwa hakuna mchezo mchezo wa kusema eti msichana fulani
gelfrendi wako, au mvulana boifrend wako, gelfrend au boifrend ndio nini?
Hakuna hata neno la Kiswahili mnaishia kulisema Kiingereza, enzi zile kabla
hamjazaliwa mtu ulikuwa na mchumba kwisha, yaani mpango wenu ni kuoana sio
kuishia gesti. Hatukuwa watu wa mchezomchezo. Enzi hizo kabla hamjazaliwa mtu akikuudhi unamtafuta mnakutana
mbashara na anapewa kipigo chake au mipasho yake uso kwa uso, sio siku hizi
anakuudhi mtu eti unaenda instagram kumpa vidonge vyake, kama sio dalili ya
woga ni nini hicho? Enzi zetu kabla hamjazaliwa ukiona nimekutumia kitu kwa
mtandao ujue hilo janga kubwa, watu ukiwaletea ujingaujinga walikuwa wanakutumia
radi kwa mtandao wa kiasili, hapo ndio utajua wengine hawachezewi, na kama unajifanya unaringia pesa
wanakutumia kitu kinanyonya pesa yako yote jeuri yako yote inaisha , hatukuwa
tunapenda mchezomchezo. Nakwambia enzi hizo kabla hamjazaliwa ilikuwa haitokei
eti mtu kaiba mume au mke wa mtu, hakukuwa na facebook au sijui whatsapp ya
kukutumia mipasho, mtu unaenda shtaki kwa babu yako halafu unangoja matokeo
baada ya siku mbili, ndugu wa mgoni wako wanakugongea mlango kukuomba msamaha
maana hapo ndugu yao kashushwa mshipa au kishakuwa chizi anaongea na mbuzi
mambo ya biashara. Hatukuwa wa mchezo mchezo. Enzi hizo kabla hamjazaliwa kulikuwa
hakuna vibaka, mtu akikuibia unaloga ukoo mzima. Nimesema hatukuwa watu wa
mchezo mchezo. Hatukuwa na gari wala baiskeli lakini tulikuwa tunatwanga kwa
mguu Dar mpaka Moro kwenda kuhudhuria harusi tu. Hatukua watu wa mchezomchezo
bwana
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE