27 April 2017

BINGWA WA NDOTO MUBASHARA


KILA  binadamu ana mambo yake mengine ya ajabu sana ukihadithiwa huwezi kuamini. Kuna mshikaji wangu mmoja wanamuziki maarufu sana, ila ana ishu yake moja watu wangejua stori yake ndio ingekuwa kichwa cha habari cha kila gazeti. Mshikaji wangu huyu mtu mmoja smati sana kabla hajatoka nje ya nyumba yake lazima ajicheki kama yuko vizuri ndio anatoka nje. Nyumbani kwake ana vioo vikubwa vitatu vyote vya kujiangalia kabla hajatoka, akiwa na unauhakika na anavyoonekana ndio anatoka. Ukijidai kumuwahi asubuhi ukimgongea kama hajajitayarisha hafungui mlango. Kuna watu walisha mzushia aeti anafuga majini, na majini yake hayataki uchafu, si unajua wabongo umbeya uko kwenye damu. Basi mshikaji huyu jina simtaji hapa maana siku hizi ukimtaja mtu jina, mabingwa wa umbeya wanamfuata mtu kwenye instagramu, wataanza kumpaka humo utadhani walikuwa nae jana kumbe hata sura wanaijulia kwenye gazeti. Unajua siku hizi umbea umegeuka dili, kuna watu wanapata umaarufu siku hizi kwa mtaji wa kuwapaka watu kwenye instagramu. Basi hapa hampati mtaji huo.   Sasa mshikaji wangu huyo tatizo lake ni staili yake ya kuota. Jamaa akipata usingizi akianza kuota tu basi huanza kufanya shughuli anazoota mubashara kabisa. Yaani akiota yuko dansini basi ataamka atashika gitaa lake na kuanza kupiga, ukimkuta utadhani yuko macho kumbe mwenzio yuko usingizini anaota hivyo. Sio mara moja anatoka chumbani kwake na kwenda mpaka mtaa wa pili na kurudi kuendelea kulala, asubuhi ndipo huwa anaamka anajikuta na matope miguuni, kutokana na kukanyaga madimbwi kwenye safari zake. Juzi juzi sasa katoa kali, mshikaji aliota kakaribishwa kwenye pati ikulu. Alivyonihadithia mwenyewe alisema alikaribishwa mlangoni na mheshimiwa Rais mwenyewe, kufika ndani akakutana Mawaziri wakasalimiana sana, akaomba sigara wakampa akavuta kisha wakaenda kula. Msosi ulikuwa wa nguvu sana, kila alichotaka alikula, mwenyewe anasema Rais alikuwa anamhamasisha ale vizuri, basi hatimae akashiba akaomba kuondoka. Kabla hajaondoka akajisikia anahitaji kujisaidia ndipo akaonyeshwa mahala pa kujisaidia, akaingia na kushusha mzigo vizuri tu. Aliposhtuka akajikuta yuko chumbani kwake kitandani, lakini chumba kinanuka harufu mbaya sana, halafu nusu ya mto mmoja aliokuwa amelalaia umetafunwa, akili ikamrudia akakumbuka ndoto aliyoota, ikawa kazi moja tu kuanza kufua mashuka na kupiga pafyumu chumba harufu ipungue, alipomaliza akaenda hospitali kumueleza dokta mkasa wake wa kutafuta mto wa sponji.

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE