Mtani
we kiboko, safari hii imenitolea mpya kabisa. Unajua tatizo la mtani wangu ni
kuwa kaingia mjini wakati kishakuwa na ndevu, lakini anataka kujifanya eti yeye
anayajua sana mambo ya mjini, na hapo ndipo anapojikuta anafanya mambo ya ajabu
sana. Mtani sikiliza ushauri, we tulia tu maana kadri unavyolazimisha mambo ndio
unachekesha zaidi. Mnakumbuka alichofanya mtani mwaka jana? Ilikuwa aibu,
alipita kwa dobi akakuta dobi kaweka kibao nje, kimeandikwa shati shilingi mia
mbili, suruali mia nne, koti alfu. Mtani wangu akaona hiyo dili kubwa, akaenda
na shilingi alfu kumi kwa dobi anataka kununua shati ishirini, suruali ishirini
na makoti matano akauze kwao, na chenji akamwambia dobi abaki nayo. Kwanza dobi
alikuwa hakuelewa, baadae akatambua kuwa jamaa ushamba unamsumbua , si ndio akamtolea
uvivu, baada ya kumlamba makofi mtani wangu ndio akamuelewesha kuwa zile ni bei
za kufua nguo mbalimbali sio bei za kununulia nguo. Mtani karudi home uso
umevimba. Sasa juzi mtani kalitia aibu kabila lake lote kwa mara nyingine.
Mtani alipita kwenye duka moja lililokuwa linauza vifaa vya umeme, akaingia na
kuuliza bei ya luninga moja aliyoiona kwenye dirisha la lile duka. Mwenye duka
akamwambia hauzi luninga, mtani
wangu akondoka huku akitikisa kichwa. Baada ya siku mbili akarudi tena pale
dukani na kuulizia bei ya ile luninga, mwenye duka akamjibu tena kuwa hauzi
luninga. Hapo ndipo mtani akaamua kuliamsha dude, akamtukana sana mwenye duka
kuwa ni mshamba hajui biashara, kwanini anakataa fedha, dude likawa kubwa
akamtukana mwenye duka matusi yaliyohusiana na familia yake, timu yake ya
mpira, kabila na mtaa wake, mambo yalikuwa makubwa mpaka yakafunga mtaa,
ikalazimika mwenyekiti wa serikali ya mtaa aite askari mgambo wa mtaa wa pili. Baada
ya kutulizana mzuka, mwenye duka akaeleza mkasa mzima, baada ya mgambo kumuuliza kwanini hauzi hiyo luninga? Ndipo
mwenye duka akajibu kuwa hicho kinachosemwa ni luninga, si luninga ni
microwave. Mgambo akamchenjia mtani wangu akalambwa makofi mengi tu, kwa mara
nyingine akarudi nyumbani uso umevimba tena. Mtani chonde chonde mambo ya mjini
tuachie wenyewe ohoo.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE