Ndugu yangu nakwambia watu wenye mapengo ni watu wa levo nyingine kabisa.
Ukimuona mtu ana mapengo mpe shikamoo.
Mtu mwenye mapengo ni mtu shujaa, usijilinganishe nae kabisa. Wiki iliyopita
niliamka fresh kama kawaida, nikatimka home na kwenda kwenye mishemishe
mbalimbali. Mida ya saa sitasita kama kawa tumbo likaanza kudai mshahara wake,
nikaingia kwa mama ntilie mmoja nikaagiza wali maharage na kikombe cha chai, mi
napenda sana chai, hata saa sita ya mchana jua la Jiji la Dar halinishawishi
kuacha kusindikiza wali maharage kwa chai, au hata chips mayai kwa chai kwangu
safi tu. Basi nikaanza kuutendea haki wali ule. Nadhani kilikuwa kijiko cha
saba au cha tisa nikiwa katika furaha kubwa si nikatafuna bonge ya jiwe kwenye
wali? Tena nikatafunia jino ambalo lilishawahi kuanza kuuma uma kidogo, ndugu
yangu hayo maumivu niliyoyasikia yalinifanya nisahau niko wapi, chozi
likanidondoka bila kupenda mwanaume. Nikainama naugulia nangojea maumivu
yapungue,wapii. Niliinuka na kuanza kuondoka bila kulipa, na mama ntilie mwenyewe hakutaka
hata kunidai alijua kuwa hilo kosa lake. Siku ikawa ndo imeharibika, nikapanda
basi niikarudi home. Nikatafuta panado nikameza nikajilaza haikusaidia kitu,
mama mmoja mpangaji mwenzangu mmbeya mmbeya akanambia ana mafuta ya karafuu nipake
kwenye jino, nikapaka nikajilaza masaa yakapita jino halitaki kupoa. Giza
likaanza kuingia mzee mzima machozi yalikuwa yanatoka bila aibu. Jirani yangu
chumba cha pili ndio akatoa shauri nikang’oe. Sikubisha maana maumivu yalikuwa
balaa, japo kichwani nilikuwa naogopa sana ishu ya kung’oa jino, lakini kwa
maumivu niliyokuwa nayapata, nilikuwa tayari kwa chochote. Jirani akanisindikiza
mpaka hospitalini, kufika kule tunaambiwa daktari wa meno hayupo mpaka kesho
yake asubuhi. Tukageuza kurudi home kichwani nawaza ntawezaje kufika mpaka
kesho yake asubuhi na maumivu makali yale? Ulikuwa usiku mrefu sana, akilini nilikuwa nawaza kuwa asubuhi mapema nawahi kung’oa jino. Alfajiri kama saa kumi na moja hivi nikapitiwa na
usingizi, nikashtuka saa mbili na nusu. Jino limetulia, linauma kwa mbali. Nikaanza kuona kuwa kung’oa sio muhimu
kiviiile. Jirani akang’ang’ania ning’oe utadhani jino lake, ‘Ohh kang’oe bwana
hilo jino litaanza kuuma tena’ na maneno mengine ya aina ile kupunguza kero nikakubali
ntaenda hospitali. Basi kweli nikaenda hospitali nikaandikisha kila kitu na kukaa kwenye foleni
ya kusubiri kumuona daktari wa meno. Ndugu yangu foleni ile inatisha, mtu mmoja
mmoja anaingia kwa dokta, halafu unasikia kilio humo ndani,'Aaaaaaaah', mwanaume mzima
analia, kisha akitoka anatoka kwa hatua ndefu utadhani ana safari ya kwenda mji
mwingine kwa miguu, kanuna, jasho linamtoka, aisee inatisha. Nikawa taratibu
nasogea kadri watu walipokuwa wanapungua, hofu nayo ilinizidi. Kiukweli
nilishindwa kuvumilia nilipoona nimefikia kuwa mtu wa tatu, niliulizia choo cha wanaume kiko
wapi, nilipotoka hapo sikugeuka nyuma mpaka nilipofika home. Jino bado linanikong’ota kila siku tena siku hizi
linaanza kuuma saa sita mpaka saba usiku, lakini kung’oa naogopa. Ndio
najiuliza hivi hawa wenye mapengo wanaokubali kung’olewa hata meno manne ni
mashujaa kiasi gani? Shkamoo wenye mapengo
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE