Nimetoka kwenye mkutano wa muhimu sana.
Mkutano wa siri sana, na kwa kweli tulichoamua kitashtua jamii. Unajua jamii
yetu hii, ina watu wakorofi sana, wakiona mtu umenyamaza basi itaanza
kukuchokoza inataka useme ukiamua kukaa kimya basi wataendelea kukufanya
uonekana fala. Sasa tumechoka tumeamua kupanga mikakati na kwa kweli habari
yetu mtaisikia muda si mrefu, maana tulishasema toka zamani, akumulikae mchana
usiku atakuchoma. Katika watu waliokuweko kwenye mkutano leo, tumebahatika kuwa na wataalamu wengi tu, najua
kwa hapa kwetu nikisema wataalamu kila mtu anafahamu nina maana gani, hawa ni
watu ambao wanaweza kufanya mambo ambayo hata wanasayansi wazungu wanabaki
wameduwaa hawajui kinachoendelea, wataalamu wetu wanaweza kusafiri kwa ungo wakatoka Dar mpaka
Mtwara na kurudi katika muda wa masaa machache tena bila kutumia petrol, wala
mafuta ya taa. Wataalam wetu wakiamua wanaweza kumshusha mtu mshipa bila hata
kumgusa, kwa kifupi wanaweza kutoa adhabu nzuri tu kwa watu wakorofi. Sasa katika moja ya maazimio makuu ya kikao chetu,
wataalamu hawa wamepewa jukumu kubwa sana la kutafuta adhabu nzuri sana kwa
watu ambao ni wameamua kutuchokoza, ni
sisi tuliosema toka zamani, ukitaka kumchinja nyani usimuangalie usoni. Kikao kilifanyika katika hali ya usiri
mkubwa, kwanza tulitumia mbinu za kiintelijensia kupeana taarifa kuhusu mkutano
huo, baada ya hapo hata ukumbi tulioutumia ulikuwa ni siri kubwa, lakini
tumeweza kukamilisha kwa mafanikio makubwa, tulishawahi kusema penye wazee
haliharibiki neno. Kwa miaka mingi sisi tumekuwa kimya sana tukiiongoza jamii
katika mambo mengi ya msingi na kutoa ushauri ambao umesaidia wakubwa na
wadogo, hatukutaka sifa wala kiki, tulitimiza majukumu yetu kiroho safi kama
mnavyosema kwa lugha ya siku hizi. Lakini bila sisi kuwachokoza , ghafla kila
mahala mmeanza kutuchokoza, kwenye mitandao mumeweka picha za kejeli, zikisema
ohh wahenga wamefanya hili, ohh huyu ndie muhenga aliyesema lile, jamani
tumewakosea nini? Sasa tunaliamsha dude, wale walioanzisha utani kwa wahenga, na wale walioendeleza utani kwa wahenga,
mjitayarishe, wataalamu wamekwisha ruhusiwa kubuni adhabu, hivyo kama ulikuwa
mmoja wapo usishangae asubuhi ukiamka ukakuta umelala bafuni, ni sisi
tuliyoleta msemo, ‘akutendae mtende’.
Wale waliotuchokoza nawashauri tafuteni wahenga waliojirani
mkajisalimishe kwani tulisema toka zamani kuwa huwa tunasamehe saba mara sabini
na saba. Ila wale wanaodharau wakumbuke tulikwisha sema mdharau mwiba huota
tende. Wahenga hatuna zaidi ya onyo la leo, kwani tulikwisha sema zamani
usimwamshe aliyelala.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE