Yaani huwezi
amini lakini kilichonitokea wiki iliyopita kimenikosesha amani kabisa, nilikuwa
nimepanga wiki hii niwe kijijini kwetu nikiwa na furaha, mambo yako tofauti
nabaki nahangaika kujificha ficha kama panya. Kosa ni kampuni ya basi moja
isiyo na upeo wa kimaadili. Mwezi mmoja uliopita mama mkwe alikuwa amaekuja
kututembelea kutoka kijijini. Alikuwa anaumwa kidogo na pia alikuwa kaja
kuwasalimia wajukuu zake. Mambo yalienda vizuri aliweza kupata matibabu na
nyumba ikawa na furaha. Sasa sisi ni kati ya watu ambao bado tunaoheshimu mila
za Kiafrika, mama mkwe ni mtu anaeheshimika sana na yeye ananiheshimu sana
mimi, kimsingi tunajitahidi kukwepana ili heshima iwepo kubwa. Ingekuwa zamani
hata kuishi nyumba moja na mama mkwe isingewezekana ingekuwa mwiko. Basi siku
za mama mkwe kukaa kwetu zikaisha na tukawa tumepanga wakati anarudi kijijini,
turudi wote maana na mimi nilikuwa na kalikizo ka wiki mbili. Pia ingesaidia
watoto wakujue kwa bibi yao, wasije wakadhani wao ni wa mjini. Nilikata tiketi
mapema ili isije ikatokea mimi na mama mkwe tukalazimishwa kukaa kiti kimoja.
Siku ya safari watoto wetu wawili, mke wangu na mama mkwe tukaingia kwenye basi
mapema tayari kwa safari ya kwenda kwetu mikoa ya kusini. Mambo yalikuwa safi,
kiyoyozi kikawashwa, viti vya mneso na tulipofika Kibaha video zikaanza kuonyeshwa. Sikuwa
na hili wala lile nilikuwa nasoma gazeti lakini nikawa nausikia muziki. Ghafla
nikasikia watoto wangu wanacheka wakaanza kumwabia bibi yao, ‘Bibi bibi ona yule kavaa kichupi kama changu’ Dah
nikashtuka, kuangalia naona video kwini ‘anamwaga lazi’. Dah balaa gani tena
hii asubuhi mapema hivi, nikakata jicho kumuangalia mke wangu namuona
kajifunika kanga usoni anajidai kalala, mama mkwe nae kaficha uso, watoto
wanazidi kushangilia, sauti zao ndio zinasikika basi zima, ‘Baba baba angalia likubwa
lizima limevaa kichupi’. Dah nikajificha nyuma ya gazeti hata maandishi siyaoni
Ukaisha wimbo wa kwanza ukaja mwingine ikawa balaa zaidi, pakukimbilia hakuna
kila wimbo wanashindana kumwaga lazi, hata wimbo mtu anaongelea namna ya kupata
pesa lakini video inaonyesha vibinti havina nguo za kutosha, basi ikawa adhabu
kubwa mpaka tulipofika Morogoro. Kufika Moro, mama mkwe akamuita mke wangu na
kumwambia wazi hawezi kusafiri na mkwe kwenye basi moja katika mazingira ya
video zile. Nikamuomba konda abadili video akajibu ile ndio wateja wanapenda.
Kukawa hakuna jinsi bali mimi nishuke au
mama mkwe ashuke, nikashuka mimi na kuruhusu familia itangulie mimi nitafute
basi jingine. Basi toka nimefika huku kijijini bado hakuna amani kati yangu na
mama mkwe, kila tukikutana tunakwepana, kikwetu kuangalia picha za aina ile
pamoja na mama mkwe na watoto si sawa kabisa, lazima mkosi mkubwa utatufikia
hata sijui nitumia tambiko gani kufuta uchuro ule
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE