Naishi
karibu na baa moja maarufu, kwa hiyo kila siku naona vituko vya walevi na
kushukuru kuwa mimi sio mmoja wao. Walevi bwana wanavituko japo wenyewe hawajui
kuwa ni vituko, na ukitaka ugomvi nao waambie kuwa wanavituko. Najua hata sasa
mlevi akianza kusoma tu hii habari atachana hili gazeti, ndio zao. Kitu cha
kwanza mlevi hakubali kuwa yeye ni mlevi, atakwambia yeye ni mnywaji, pamoja na
kuwa hata anachokunywa kimeandikwa kuwa ni kilevi bado atakubishia kuwa yeye si
mlevi. Walevi wako wa aina nyingi sana, lakini kimsingi pombe humfanya mtu
ajione yeye yuko tofauti na kawaida. Hivyo mtu ambaye hajui Kiingereza akilewa
anajiona anajua sana lugha hiyo, na hivyo usishangae akianza kusisitiza kuongea
Kiingereza japo hajui. Kwa msingi huohuo, wako wale ambao wanajijua hawana
uwezo wa kupigana lakini akilewa anajiona anauwezo wa kumpiga kirahisi Meiweza
na hivyo walevi wa aina hii huwa wanapenda sana kuanzisha ugomvi, ili wapate
nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Shida inakuja wakati mlevi anapojiona kuwa yeye
ni mwalimu wa kung fu, nyie wote mnamuonea huruma hata kusimamama hawezi wakati
yeye anajiona anaweza kuwapiga watu wote kung fu kirahisi kama kwenye video.
Juzi usiku wa manane polisi wamekuja kuwatimua walevi waliopitiliza muda, mmoja
wao akadai amesoma sana sheria na kuanza kutaja vifungu vya sheria
vinavyomruhusu binadamu kunywa pombe wakati wowote, na kugoma kupanda
karandinga, akaishia kupigwa virungu vya kwenye visigino mwenyewe akapanda gari
la polisi. Halafu kuna walevi wadada waliowatoroka wapenzi wao, hawa
wanachekesha kweli, wakipigiwa simu kwanza hutimka mbio na simu kukimbia kelele
za muziki, wala hawafiki mbali kwa akili zao wanajua muziki hausikiki, utasikia
‘Bebi vipi mbona unapiga simu wakati nimelala?’ Baada ya sekunde utajua tu kuwa
aliyeupande wa pili anasikia muziki na ameulizia, mdada mlevi utasikia ‘Huo
muziki unatoka nyumba za jirani kuna kigodoro’ Hapo anakuwa kajichanganya maana
Zilipendwa ya Chibu inasikika wazi. Ila raha kubwa ni pale mlevi kaishiwa
lakini hataki kuondoka kaunta, msikilize anavyotamba kuwa anapesa benki zote za
mjini, hapo anadhani eti ndio atakopeshwa kwa mali kauli hiyo.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE