MTANI wangu sasa
amevuka mpaka, yaani kila nikimkumbuka nacheka mpaka ninashindwa kupumua. Niko
na mtani wangu hapa kwenye kidispensari mtaani kwetu watu wote wananishangaa kwanini namcheka
mgonjwa. Ngojeni niwape stori nzima Unajua mtani kaja kunitembelea mjini ili
asafishe macho. Alinipigia simu kuwa anataka akirudi kijijini awe na stori za
kuhadithia. Kwlei alipofika nimemzungusha sehemu nyingi za muhimu. Nimesha
mpeleka baharini akachota maji ya bahari kayaweka kwenye chupa atarudi nayo
kijijini kwao, nimeshampeleka kuliona daraja la Kigamboni, na nimepeleka klabu
mara mbili. Nimemuingiza kwenye lifti akapanda mpaka ghorofa ya kumi,
nimempandisha kwenye ngazi zinazotembea, ameanza kuwa mjanjamjanja. Kama siku
tatu zilizopita nikampeleka kula kwa mama ntilie yule wa Kijitonyama ambae ni
bingwa wa pilipili kali. Mtani wangu alikula biriani kwa mara ya kwanza katika
maisha yake na kusifia sana wali wa rangirangi kama alivyokuwa akiuuita
mwenyewe. Sasa jana mtani kaenda peke yake kwa mama ntilie, baada ya kula wali
wa rangi rangi, akaona kashata za rangi nzuri akazitamani, akaulizia bei
alipoambiwa akanunua kashata ishirini akafungiwa na kurudi nazo nyumbani. Mtani
wangu akazificha vizuri kashata zile na
kuanza kudokoa moja moja akawa anatafuna kwa siri. Haikuchukua muda akamaliza
kashata zote. Niliporudi nyumbani
nimemkuta mtani kalala kwenye mkeka nje ya nyumba, nikashangaa maana sio tabia
yake, baada ya kumuamsha aliamka lakini akawa amelegea sana, hata macho yake
yalikuwa yamelegea kama vile kalewa. Nikadhani labda malaria nikamuuliza kama
anaumwa akaninijibu kwa sauti ya kinyonge kuwa haumwi kachoka tu. Kiukweli
nikawa na wasiwasi, dalili zote zilionyesha hakuwa salama. Na ni wakati huohuo
alipoanza kutimka kukimbilia chooni, ikawa kila dakika tatu anarudi chooni,
anadai tumbo limechafuka namuuliza alikula nini hajibu. Ila alikuwa anazidi
kulegea nikaona asije akanifia ndugu zake wakanila nyama, ndio nikamleta hapa
dispensary. Dokta kamuuliza mtani wangu alichokula ndipo kwa aibu akalazimika kueleza
kuwa alinunua kashata nyingi na amekula zote. Mi nikamuuliza alinunua wapi zile
kashata, akajibu kule kwa mama ntilie wa Kijitonyama, hapo ndipo nilipoanza
kucheka karibu nivunje mbavu. Ni kweli mama ntilie wa Kijitonyama anatengeneza
kashata, lakini kashata zake si za nazi na wateja wake ni wanawake tu maana
kashata zake ni za kungu. Ndio maana mtani macho yamemlegea, kafakamaia kashata
20 za kungu dahh
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE