23 November 2017

MTANI wangu sasa amevuka mpaka, yaani kila nikimkumbuka nacheka mpaka ninashindwa kupumua. Niko na mtani wangu hapa kwenye kidispensari mtaani kwetu  watu wote wananishangaa kwanini namcheka mgonjwa. Ngojeni niwape stori nzima Unajua mtani kaja kunitembelea mjini ili asafishe macho. Alinipigia simu kuwa anataka akirudi kijijini awe na stori za kuhadithia. Kwlei alipofika nimemzungusha sehemu nyingi za muhimu. Nimesha mpeleka baharini akachota maji ya bahari kayaweka kwenye chupa atarudi nayo kijijini kwao, nimeshampeleka kuliona daraja la Kigamboni, na nimepeleka klabu mara mbili. Nimemuingiza kwenye lifti akapanda mpaka ghorofa ya kumi, nimempandisha kwenye ngazi zinazotembea, ameanza kuwa mjanjamjanja. Kama siku tatu zilizopita nikampeleka kula kwa mama ntilie yule wa Kijitonyama ambae ni bingwa wa pilipili kali. Mtani wangu alikula biriani kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kusifia sana wali wa rangirangi kama alivyokuwa akiuuita mwenyewe. Sasa jana mtani kaenda peke yake kwa mama ntilie, baada ya kula wali wa rangi rangi, akaona kashata za rangi nzuri akazitamani, akaulizia bei alipoambiwa akanunua kashata ishirini akafungiwa na kurudi nazo nyumbani. Mtani wangu akazificha vizuri kashata zile  na kuanza kudokoa moja moja akawa anatafuna kwa siri. Haikuchukua muda akamaliza kashata zote.  Niliporudi nyumbani nimemkuta mtani kalala kwenye mkeka nje ya nyumba, nikashangaa maana sio tabia yake, baada ya kumuamsha aliamka lakini akawa amelegea sana, hata macho yake yalikuwa yamelegea kama vile kalewa. Nikadhani labda malaria nikamuuliza kama anaumwa akaninijibu kwa sauti ya kinyonge kuwa haumwi kachoka tu. Kiukweli nikawa na wasiwasi, dalili zote zilionyesha hakuwa salama. Na ni wakati huohuo alipoanza kutimka kukimbilia chooni, ikawa kila dakika tatu anarudi chooni, anadai tumbo limechafuka namuuliza alikula nini hajibu. Ila alikuwa anazidi kulegea nikaona asije akanifia ndugu zake wakanila nyama, ndio nikamleta hapa dispensary. Dokta kamuuliza mtani wangu alichokula ndipo kwa aibu akalazimika kueleza kuwa alinunua kashata nyingi na amekula zote. Mi nikamuuliza alinunua wapi zile kashata, akajibu kule kwa mama ntilie wa Kijitonyama, hapo ndipo nilipoanza kucheka karibu nivunje mbavu. Ni kweli mama ntilie wa Kijitonyama anatengeneza kashata, lakini kashata zake si za nazi na wateja wake ni wanawake tu maana kashata zake ni za kungu. Ndio maana mtani macho yamemlegea, kafakamaia kashata 20 za kungu dahh 

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE