Toka
nilipokuwa mdogo nilikuwa naambiwa na wakubwa, ‘Usimcheke mwenzio akipata
tatizo’, kiukweli nimekuwa najitahidi sana kufwata ushauri huo, lakini mara
nyingine bwana nimekuwa nashindwa kujizuia kuna matatizo mengine
yanachekesha mno. Yaani kama ni rafiki
yako kaja kukuhadithia, ingawa anatoka machozi, we unamsikiliza kwa makini
halafu unamwambia unaenda bafuni ukifika huko unacheka halafu unarudi na sura
flani siriaz, kisha unaendelea kumpa pole.
Sasa ngojeni niwambieni kisa fulani kimemtokea rafiki yangu mmoja mjanjamjanja wiki iliyopita, yaani bado
nacheka japo jamaa yangu akitokeza ghafla nakuwa siriaz, akijua namcheka
patakuwa padogo nakwambia.
Huyu jamaa
yangu ana tatizo moja kubwa sana, yaani kama vile haamini kuna Mungu, akiamka
hana hela basi ataenda kwa mganga akaangalie nani kasababisha mkosi wa namna
ile , akipata pesa lazima aende kwa mganga amtengeneze ili wabaya wasije
wakazikwapua zile pesa kimiujiza. Akitaka kusafiri lazima akaague, akitaka
kupata mpenzi mpya lazima aende kwa mganga, mimi nimeshamsema nimechoka. Najua
lazima kishaenda kunicheki kwa wataalamu wake kama mimi nampenda au fiksi hilo
nina hakika. Sasa siku chache zilizopita
akapata mesej ndefu kwenye simu yake, meseji ilionekana kama imekosea namba,
ilionekana kama meseji imetoka kwa babu mmoja inaenda kwa mjukuu wake. ‘Mjukuu
wangu hebu muulize rafiki yako kwanini hanilipi pesa yangu? Mimi nimemsaidia
nimempa yule jini mpole kwa laki tano tu na ameweza kwa muda mfupi kumpa mabasi
matatu na nyumba nne, sasa kwanini hanilipi? Mwambie zile nyumba zinaweza zote
kupukutika, mkumbushe alipe deni upesi niishukuru mizimu’. Nakwambia jamaa akaja kwangu macho yamemtoka, bila hodi
wala salamu akaanza,’Bradha Mungu kanikumbuka, yaani kuna meseji ilikuwa iende
kwa mtu mwingine imekuja kwangu na hii ndio itanitoa kwenye umasikini’. Basi
akaanza kunisomea ujumbe ule, mi nikamuuliza sasa wewe unahusika vipi hapo?
Akacheka kwa dharau na kunambia kuwa mie akili yangu iko sloo sana, akaniuliza
kwa dharau ‘Hivi hujui hapa nimeshapata namba ya huyu babu?, kwa hiyo na mimi
namtafuta ili anipatie na mimi langu jini nitajirike’. Duh kifupi nilijaribu
kila njia kumkanya hakusikia. Sasa toka
juzi ananinisumbua huku analia machozi, eti aliwasiliana na yule babu vizuri,
akaambiwa atume laki tatu za kufanyia kafala, baada ya kutuma tu pesa ile namba
ya babu haiku tena hewani. Sasa jamani kwanini nisicheke?
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE