8 July 2012

Unajua kwanini nyani hana ngozi kwenye makalio?

Hadithi hadithi, hapo zamani za kale kulikuweko na sungura aliyekuwa na familia yake ya mke na mtoto mmoja, akawa ana hamu sana ya kujenga nyumba ya kuishi na familia yake. Akazunguka akitafuta mahala pazuri pa kujenga nyumba hatimae akapapata, akapasafisha siku nzima akajitayarisha kwa kuweka nguzo za awali za nyumba yake. Kumbe simba nae alikuwa na tatizo hilo hilo, nae akazunguka kwa mshangao akakuta mahala pazuri alipapenda pamekwisha safishwa akaamua kuanza kujenga alifanya kazi nzuri siku hiyo ikabakia kuweka paa. Sungura alipokuja baada ya siku moja akashangaa pameshajengwa hivyo akamshukuru Mungu na kuamua kuweka paa, nyumba ikawa tayari. Siku alipokuja kuleta familia yake akashangaa kukuta simba nae yupo na familia yake, wakasalimiana na baada ya majadiliano wakakubaliana kuwa nyumba ile waliijenga pamoja wakagawana vyumba. Mapema kabisa sungura alijua ujirani huu ni wa hatari sana, hivyo akapanga na mkewe njia ya kumtoa simba. Usiku wa manane akamuamsha mkewe kwa sauti,'Mke wangu ile mifupa ya simba tuliyemla wiki iliyopita iko wapi?' Mkewe akajibu, 'Si ulisema niiweke utampa mbwa wetu?'. Sungura,'Ahh okay, nilidhani imekwisha nikamtafutie mbwa wangu simba mwingine'. Simba kusikia vile alimuamsha mkewe na wakakosa raha kabisa kiasi cha kuhama jua la kwanza kwa kuogopa kuliwa na sungura. Wakiwa wanahaha porini, mvua ikaanza wakajikunyata chini ya mti kwa baridi, nyani akapita, akamuuliza Simba,'Mzee vipi tena mbona uko kwenye mvua huna raha?', Simba akamwambia nyani kuwa hana nyumba kwa kuwa amekimbia nyumba kukwepa kuliwa na sungura, nyani akacheka sana,'Sungura kumla simba? sijawahi kusikia hebu nipe mkasa mzima'. Simba akahadithia mkasa wote na kumuwacha nyani anacheka  sana,'Sasa mzee, sungura kakudanganya, twende naenda kumtandika mikwaju mbele yako hana adabu kutisha wakubwa'. Msafara ukaanza kurudi alikokuwa sungura. Sungura alikuwa nje ya nyumba yake akamuona nyani akiongoza msafara wa simba na familia yake, akajua dili limebumbuluka. Walipofika karibu sungura akwahi kumkaribisha nyani,'Aise bradha nyani, aksante sana sikutegemea kama ungeweza kuwaleta kama ulivyoniahidi'. Simba kusikia hivyo akapaniki,'Haaa nyani kumbe umeniuza?' Alichofanya ni kumkwangua nyani ngozi ya makalioni nakukimbia na kupotea. Na ndio maana mpaka leo nyani hana ngozi makalioni

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE