Enzi hizo wakati bado ningali mtoto, kila mtaa ulikuwa na
kiwanja cha kuchezea, tena kikubwa maana unaweza ukakuta michezo mitatu ya soka
na michezo miwili ya netiboli inaendelea kwa wakati mmoja, achana na wale
waliokuwa wakicheza mdako, kiboleni, gololi na hata kufukuzana tu. Kwenye soka
enzi zile, tulikuwa na sheria zetu za kuongoza mchezo huo. Sheria zetu hazikuwa
zinafwata za FIFA, kwanza wakati huo hata hilo neno FIFA tulikuwa hatulijui.
Wenyewe tulijitengenezea amri ambazo hazikuandikwa popote lakini kila mtu
alikuwa anazijua kimoyomoyo. Tulikuwa na amri zetu kama kumi hivi. Kwanza
wakati huo mipira yenyewe ilikuwa tabu kupatikana hivyo wengi tulikuwa
tunatengeneza wenyewe kwa kufunga makaratasi na kuanza mechi ambazo kupumzika
ni uamuzi tu, inawezekana mtu kishafungwa 20 kwa kumi na mbili, basi mnaamua
kupumzika. Lakini ilikuwa ikitokea mwenzenu mmoja wazazi wake wako vizuri
wakamnunulia mpira wa kweli, hapo basi kidogo kulikuwa na taratibu mpya katika
kuchezea mpira ule. Tulijitengenezea amri kama kumi hivi. Amri ya kwanza
ilikuwa mwenye mpira ndie anaeamua nani atacheza, hivyo kama uliwahi kumnyima
kashata au andazi ni wazi huchezi. Amri ya pili ilikuwa mtoto
bonge ndie golikipa, hilo lilikuwa halina ubishi. Tatu ni kuwa wachezaji wazuri
ndio wanaochaguliwa kwanza na mwenye mpira kuwa watakuwa timu yake. Amri ya nne
ilikuwa kukiwa na penati ruksa kubadilisha kipa kama kipa
wenu hamumuamini. Amri ya tano ya mpira enzi zetu ni kuwa ukipiga
mpira kwa nguvu au kwa mandochi yaani kwa vidole, kumbuka tulikuwa hatuvai
viatu, basi mwenye mpira ana ruksa ya kukuonya au kukukataza usicheze. Amri ya
sita ya mpira enzi zetu ni kuwa usipochagia hela ya kujaza upepo mpira utapigwa
marufuku kucheza. Amri ya saba ilikuwa hakuna marefa wala washika
vibendera, na mpira unachezwa mpaka kuzunguka goli, ila mwenye mpira anaweza
akageuka refa wakati wowote na atakachosema lazima kiwe. Kati ya amri muhimu
ilikuwa ni ile ya nane, si ruhusa kabisa kumkaba mwenye mpira, hiyo
ni faulo. Ya tisa ni kuwa ukitoboa mpira unalipa. Mwisho ni kuwa mwenye
mpira akikasirika au akiumia au akiitwa na mama yake ndio mwisho wa mechi.

No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE