10 December 2016

NDOA BILA SENDOFF ETI SIO NDOA

Unajua hapa Bongo kuna watu wakorofi sana, kuna watu wanajifanya wao wako kama serikali. Yaani wakisikia chochote kimefanywa na serikali na wao wanataka kufanya pia, sijui wakoje? Tabu yake mambo wanayofanya ndio yale wastaarabu wanaita kudandia treni kwa mbele, mambo ya uchizi uchizi tu. We fikiria, juzi zilienea habari kuwa kama hukusoma fom siksi, basi diglii yako feki, sasa imekuwa tabu mtaani nakwambia. Binamu yangu kaenda kuomba kazi ya ulinzi kaulizwa kiwango cha elimu yake, akawambia alimaliza la saba, akaulizwa kama alisoma nasari, alipowaeleza kuwa hakupitia huko, wakamwambia hawezi kupata kazi maana cheti chake cha darasa la saba kitakuwa feki. Jamani nasari na cheti cha darasa la saba wapi na wapi? Kama sio uchizi ni nini hicho? Kali zaidi imetokea huko kijijini kwetu, ndugu yangu Abuu alikutana na binti mrembo wakapendana na wakapanga kuoana. Abuu akaanza mipango ya ndoa kwa kufuata taratibu zote za awali, akajitambulisha kwa wakwe, kisha akatafuta mshenga na kukamilisha kutoa mahari, baada ya muda si mrefu harusi ikafanyika wapenzi hawa wawili wakawa mtu na mkewe. Katika kutafuta maisha Abuu akaamua kuhamia mjini kutafuta kibarua, Mungu si Athumani akapata kibarua, akapata chumba cha kupanga kwa mama mmoja mwenye maneno mengi, akaona bora amuite mke wake mpenzi maisha yawe ya furaha zaidi. Kitendo cha kumleta mkewe kikaanzisha maneno toka kwa mama mwenye nyumba. Akanza kulalamika kuwa nyumba yake inageuzwa dangulo. Awali jamaa yangu hakujua kuwa yale maneno yalimhusu yeye. Ila siku moja ikawa dhahiri kuwa vijembe vile ni vyake. Akaona amuulize mama mwenye nyumba kwanini ana mnyanyasa vile. ‘Mama vipi nasikia unalalamika kuwa nimegeuza nyumba yako kuwa dangulo, sijakuelewa’ . Yule mama akawa utadhani ndio alilokuwa akilingojea maisha yake yote. ‘Ehee baba nilikupangisha chumba nikakuona wewe ni mtu mtulivu sasa naona umeleta changudoa nyumbani kwangu’. Jamaa akaja juu,’Mama nitake radhi huyo ni mke wangu nimemuoa kwa taratibu zote huwezi kumuita changudoa’. Ilikuwa kama vile yule mama hakuamini, akauliza ‘Ndoa yenu ilikuwa a sendoff?’ ‘Sendoff ya nini? Kijijini kwetu hakuna kitu kama hicho’ Looo hapo ndipo uchizi ukaingia, yule mama akapiga kigelegele, ‘Unaona nilijua tu, hapo hakuna ndoa. Ndoa bila sendoff ni ndoa feki’ Dahhh kweli uchizi unaongezeka

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE