7 January 2017

2017 SITAKI TENA SIMU ZA KUPANGUSA


Haya tumshukuru Mungu 2017 ndiyo hiyo tumevuka. Tunanza na mikakati ya kuishi vema 2017. Mimi nina mipango mikakati kibao, ngoja niwamegeeni michache labda itawasaidia. Mkakati wa kwanza nikubadilisha taratibu zangu za mawasiliano. Wakuu natangaza kuwa hamtaniona tena whatsapp, wala insta wala facebook. Ile simu yangu ya kufuta nauza tena nauza bei rahisii. Nimegundua ile simu ina jinni la kumaliza pesa, jinni la kumaliza muda, na wote hao wakishirikiana na jinni mahaba. Yaani kuna jini mle linakulazimisha uwe na vocha muda wote masaa 24, yaani linakufanya hata ukiumwa badala ya kwenda kununua dawa we unaenda kununua vocha ili tu uposti kwenye whatsapp na facebook kuwa unaumwa, sasa akili gani hiyo. Yaani ukiamka bila credit kwenye simu unakuwa kama mgonjwa, unahangaika kutafuta pesa hata ikiwezekana ujidhalilishe uombe watu wengine wakuunganishe. Jini baya sana lile. Hili jini la kumaliza muda linahakikisha akili yako yote imekaa inangojea meseji za whatsapp, usiku na mchana, kabla hujalala lazima ucheki nani katuma ujumbe, na kama ukikuta grup lina stori unaweza ukajikuta uko macho saa tisa za usiku unajibishana na mtu yuko Marekani ambako mwenzio kule mchana jua linawaka. Hata kama unaendesha gari hili jinni linakulazimisha uwe unachat, yaani badala ya kuwaza mambo ya kutafuta pesa unahangaika shingo umekunja, unachat na watu kumi kwa mpigo. Huku insta lazima ucheki kama kuna mtu kamtukana supasta wako ili timu yenu mmchangie kumpasha, sasa jambo la ujinga ni kuwa supasta mnaemtetea wala hawajui wala hana taimu na nyinyi sasa si bangi hizi? Halafu kuna hili jinni mahaba, hili linakurahisishia kupata wapenzi wengi kwenye simu halafu wote kazi yao ni kukuomba uwaunganishe muda wa maongezi, hebu fikiria mtu una wapenzi kumi kila mmoja anaomba muda wa maongezi, si kutiana umasikini huku? Unamuandikia mmoja  I miss you halafu una kopi na kupesti kuwatumia wote tisa kila nusu unakazi hiyo, hapana imetosha nauza hii simu ya kupangusa, naanza 2017 na ka nokia tochi hata kama yuzdi tu, mradi niwe huru na hawa majini.

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE