18 January 2017

WANAMUZIKI NA WANASIASA KUMBE NDUGU KABISA, haki ya mzungu tena



Nilikuwa nimekaa kwenye kijiwe kimoja wanapouza pombe za kikwetukwetu, nateremukisha plastiki moja baada ya jingine, mambo ni mazuri sana siku hizi, maana hata hivi vijiwe vyetu vimeboreshwa kuna luninga za fletskrin. Hata sisi sasa tunaona laiv hotuba za wanasiasa na kupata burudani ya kusindikizwa na Bongofleva wakati wa kushushia hii kitu ya asili.
Ujue ukiwa unakunywa hivi vitu akili inachangamka, mizimu inaamka na kuanza kukupa maelekezo mbalimbali yenye manufaa, we fikiria  unaweza ukaanza kinywaji hujui Kiingereza lakini baada ya plastiki tatu Kiingereza iz spiking iz vere izeee, yaani kinakuwa rahisi kabisa. Au unaanza hujui kabisa kucheza lakini baada ya plastiki kadhaa unakuwa na uwezo wa kucheza show ambalo wacheza shoo wa  Wasafi Classic wakikuona wanakuibia staili. Hizi ni baadhi ya faida chache za pombe za  kikwetukwetu, faida ambazo Taifa halijazitumia, hebu fikiria yaani niliachwa kuoneshwa kwenye loyotua bila sababu. Enewei hapa akili imeshachangamka nimegundua kumbe wanamuziki na wanasiasa ndugu kabisaa, tena inawezekana hawa ni pacha. Kwanza kabisa wote wanaishi mjini kwa kutunga mistari. Ila huyu ndugu mmoja huwa anaweka biti kwenye mashahiri yake hivyo anayosema yanautamu unajikuta unacheza wakati unamsikiliza. Nimefanya risachi nikaanza na babu za hawa Bongofleva, hebu kumbuka kale kawimbo ka Dada Asha iz of Tabola Jazz Band, ze mwimbaji aliahidi kumnunulia Asha ndege, sio njiwa nooo elopleni na wale myuzishen wa Ulafiki Jazbendi wakawa na kawimbo kao eti maisha mjini hayafai wanaenda Gezaulole makao mapya kulima. Watu wakakubali na kucheza sana mistari hiyo, wakati myuzisheni anamuahidi  Asha kuwa atamnunulia elopleni, yeye mwenyewe hata hela ya kula kesho hajui itakakotoka dah, walipokuwa wakihimiza watu kwenda kijijini kulima hata jembe walikuwa hawajui linashikwaje. Ukimpa myuzishen jembe analishika kama kakumbatia gitaa la bezi hahahahaha. Enewei hao ndio wanamuziki bwana na mpaka leo hawajabadilika ila wameboresha uwongo wao siku hizi unasindikizwa na video, wote wana mabinti wakali, magari ya kifahari nguo za bei mbaya na nyumba za ghorofa, wakimaliza shuting wanarudi geto kwenye godoro chafu hahahahaha. Sasa ndugu zao wanasiasa nao wana mistari mikali lakini bila muziki, hawa bwana wanaweza kukwambia nipe kura zako ntakuletea barabara, utaishi maisha kama Ulaya, kila mtu atakuwa na hela mfukoni, magonjwa yatakwisha, dawa ya korona itatengenezwa Nachingwea na kugawiwa bure nyumba hadi nyumba. Mwenyewe utajikuta unapiga makofi. Na wao siku hizi wameboresha promo zao, zinaonekana mpaka kwenye luninga, ukiingia mkenge uwachague ndio huwaoni tena mpaka baada ya miaka mitano wanapokuja kukupa mistari mingine iliyoboreshwa zaidi. Ngoja niongeze plastiki jingine, nami nijione nina ngumi kama Tyson, nikawashushie kipigo wale vibaka mtaani kwetu, naenda kuwapiga mpaka waombe poo, unajua Jek Chen mtoto wa mama yangu mdogo? .  

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE