Duniani
kuna watu wana roho mbaya sana jamani dah. Yaani mtu anakufanyia kitu kibaya
unaumia yeye ndio kwanza ananunua soda anakunywa anakuangalia jinsi unavyoteseka.
Halafu binadamu tuna kamsemo fulani eti mtu mkatili namna hii ana roho ya
kinyama, yaani tunawaonea kabisa wanyama, huwa hawana roho mbaya. Ila binadamu
khaaa. Leo niongelee dereva wa basi moja ambae alinifanyia mtima nyongo
sitasahau, niliapa sipandi tena mabasi ya kampuni yake. Siku hiyo nimeamka
mapema nikawahi basi naelekea mkoani kwenye dili zangu. Safari ikaanza vizuri
kama kawaida video za muziki wa Bongofleva zikaanza kuonyeshwa, kausingizi
kadogo kakaninipitia. Niliposhtuka tulikuwa tumeenda mbali kidogo kwa mbali
nikasikia kama vile nataka kwenda jisaidia, nikaona poa ntasubiri basi
litakaposimama nijinafasi. Baada ya masaa mawili hali yangu ikawa sasa ngumu
kidogo, nikasimama na kwenda kwa dreva na kumtaarifu hali yangu. Akanijibu
kistaarabu, ‘Subiri tunasimama hapo mbele baada ya dakika chache’. Nikarudi
kwenye kiti, dakika arobaini na tano baadae hakukuwa na dalili yoyote ya basi
kusimama, hali yangu ilikuwa tete sikuwa hata na nguvu za kusimama kumwendea
dreva maana nilijua nikisimama tu nitaachia. Nikampigia kelele konda, akanijibu,
‘Jamani si umeambiwa tutasimama muda si mrefu? We mzee vipi?’ Jamani jasho likaanza kunitoka,
ningekuwa mtoto mdogo ningeshaachia , nilikuwa nahangaika kwenye kiti vibaya
sana, video naiona naisikia lakini hata sijui ilikuwa inaimba wimbo gani. Kila
sekunde kwangu ilikuwa mwaka, na gari likijirusha ilikuwa kama vile sasa ndio
najiachia. Nikaona heri nitambae mpaka kwa dreva. Nikafika mbele na kumuomba,
‘Baba chonde naumbuka mwenzio’. Alichofanya ni kubadili gia na kunambia subiri
kidogo mzee, kuna kituo cha mzani hapo mbele huwa tunasimama, utamaliza mambo
yako huko. Nikaona isiwe tabu kama kuumbuka nishaumbuka, nikajiachia palepale
mbele ya dreva. Yaani uzito wote ukanitoka nilikuwa kama nimeshusha mzigo wa
tani kumi. Konda na dreva wakaanza matusi yao wala sikuwasikiliza, nikawa
natabasamu kwa raha, nikarudi kwenye kiti changu suruwali imelowa, abiria nao
wengine wanatukana wengine wananihurumia, potelea mbali mradi nimerudi kuwa
binadamu huru tena.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE