11 February 2017

MIZIMU ITAAMUA


Teknolojia mpya zinatufanya tuwe watu wa ajabu ajabu. Unaweza ukaingia hotelini watu wanakula lakini mkono mmoja wameshika simu, wako bizi wanachati, hapo ndipo uatashangaa mtu kashika tonge la ugali mkononi lakini halipeleki mdomoni wala halishushi liko hewani tu, akili yote kwenye simu halafu anacheka peke yake. Kuna wajinga wengine wanavaa iafon masikioni, wakiwa wamefungulia muziki mkubwa wanatembea barabarani wanakoswakoswa na magari kama vile hawasikii honi, uchizi mtupu. Juzi sinakaingia ofisi flani nilikokuwa na shughuli nyeti, kama kawaida nikamkuta mdada ambaye ndie anaruhusu watu kumuona bosi au la, mdada alikuwa nyuma ya bonge la kompyuta. Nikamuuliza, ‘Bosi yupo?’ Bila kuniangalia sura akasema subiri kidogo’ Nikakaa kwenye makochi mazuri napigwa na kiyoyozi. Nikaanza kusoma soma vijigazeti mpaka nikavimaliza, nikainuka kumucheki yule mdada kuona kama kamaliza kazi yake anisikilize, nikawa nashangaa, alikuwa bizi sana kwenye kompyuta yake, mara atabasamu, mara anune, mara asonye. Nikajaribu kumkumbusha tena kuwa nipo akanijibu kwa ukali , ‘Huoni niko bizi, nimesema subiri, we mzee vipi?’ Nikawa mpole. Kwa bahati bosi akatoka, kuniona tu, akaanza, ‘Shikamoo mzee, loh mbona hujanambia uko hapa samahani sana mzee wangu ningejua uko hapa ningekwisha kutoka’. Yule mdada kuona bosi wake kawa mdogo vile ndipo akagundua kumbe kisha likoroga. Bosi wake akamuuliza, ‘Kwanini hukumruhusu huyu mzee kuniona?’ wakati huo akazunguka kuangalia mdada alikuwa na afanya kazi gani. ‘Yaani we uko kwenye fesibuku Mzee wangu umemchelewesha kuingia, unajua kuwa mali yote hii nilipata kwa hirizi za huyu mzee?’ Bosi akanigeukia mimi, ‘Mzee wangu kosa ni la huyu binti mi siwezi kukuvunjia heshima, unanijua toka niko mdogo sijawahi kukuvunjia heshima mzee wangu nisamehe’. Nikamuangalia yule binti kisha nikajibu tu ‘ Usiwe na wasiwasi kijana wangu nimekusamehe, ila kuhusu huyu binti ntakapozungumza na mizimu leo usiku ndio ntaambiwa cha kufanya, kama nimuoe au awe sadaka ntapata jibu kwa mizimu’ Kwa jinsi uso wa yule binti ulivyokuwa, sidhani kama atamdharau mgeni atakaekuja kuja pale tena.

No comments:

Post a Comment

SEMA USIKIKE