HAYA
tena ndege mpya hizo, hatimae tutaweza kusafiri kwenda makwetu kwa kutumia
ndege, makofi tafadhali. Mambo si ndiyo haya, siku ya uzinduzi na mimi
nilikwenda eapot, nizione zile ndege zetu kwa macho yangu, ujue nimechangia
kununua zile ndege, si unajua zimenunuliwa na kodi za wananchi na mimi ni
mwananchi. Kimsingi ilitakiwa jina langu nalo liandikwe kwenye kadi ya ndege,
ya kuonyesha mwenye mali lakini nimeikabidhi serikali kodi yangu hivyo
nimeiruhusu serikali iandike jina lake kwa kipindi cha mpito. Siku Mkuu wa Kaya anazindua ndege, nilikuwa
mmoja wapo wa wananchi ambao tulipanga foleni kuingia ndani ya ndege na kukagua
kama kodi yetu imenunua kitu sahihi, nashukuru kila kitu kipya, viti vyake raha
full kunesa. Kwa sasa nangojea ratiba itoke nijue ndege zitakuwa zinaenda wapi,
hapo ndipo ntatafuta safari. Lazima nipande ndege mwaka huu. Nina rafiki zangu
Mwanza, Njombe, Singida, Ntwara, Thame, Arusha Chini, kote lazima niende na
ndege. Ila kuna kitu muhimu niwataarifu, ndege sio kama mabasi haya ya kwenda
mikoani, ndege kitu kingine bwana , ndege kitu cha heshima, wakati unapanda
ndege mtu lazima ujitayarishe kisaikolojia na pia kuwataarifu ndugu na jamaa na
mtaani wajue ishu hiyo. Ngoja nikupe mfano, ukiwa unapanda daladala za kwenda
kule kwa wale jamaa ambao huwa wanaingilia madirishani, utakuta kuanzia konda
kavaa hovyo, dereva kavaa hovyo, basi halijaoshwa mwezi wa pili sasa, viti
vibovu, hivyo msafiri na wewe ukiwa hovyohovyo poa tu. Halafu kuna mabasi siku
hizi unanunua tiketi mapema, ukiingia kuna konda wa kike msafi, dereva kavaa
tai, basi safi hivyo na wewe unajipanga usije kuchafua basi la watu. Sasa ndege
ni kitu kingine, kila kitu kisafi mara kumi, wahudumu warembo, mapailoti
mahendsam, unaweza ukapata bahati ya kuoa au kuolewa kutokana na safari moja tu
ya ndege, sio mchezo. Hivyo basi siku chache kabla ya kupanda ndege lazima
kuanza matayarisho. Unafanya shopping ya ukweli viatu vipya, pafyumu kali,
sanduku jipya la magurudumu, kimsingi kila kitu kipya cha kupandia ndege mpya.
Suti kali kwa wanaume, akina mama saluni ni muhimu, unaingia kwenye ndege
unapendeza, ila onyo tafadhali madera sio fresh kwenye ndege mpya.
No comments:
Post a Comment
SEMA USIKIKE