Leo sijui kwanini nimekumbuka hadithi moja ya Abunuwasi.
Hapo zamani za kale Abunuwasi alimuendea mfalme akamwambia anaweza kumshonea suti
ya thamani sana ambayo wenye dhambi watakuwa hawaioni na wasio na dhambi tu
ndio watakuwa wanaiona. Mfalme akampa kazi Abunuwas ya kutengeneza suti ya aina
hiyo kwa ajili yake. Kwa siku kadhaa Abunuwasi alijifungia katika chumba akawa
bizi anashona suti ya mfalme. Baada ya siku tatu, mfalme akamtuma msaidizi wake
akaangalie kazi inavyoendelea, yule msaidizi akaingia chumba alichokuwa
akishonea Abunuwasi lakini hakuona kitu japo alimuona Abunuwasi akifanya
vitendo kama vile yuko bizi anashona nguo. Msaidizi akamwambia Abunuwasi,
‘Nimetumwa na mfalme niulizie umefikia wapi?” Abunuwasi akamjibu, “Kwani we
huoni jinsi suti ilivyoanza kupendeza, ila bado namalizia nguo nyingine nataka
kuanzia nguo za ndani ziwe ni hizi za kitambaa ambacho hakionekani kwa wenye
dhambi”. Hakika yule msaidizi alikuwa haoni kitu lakini ili aonekane hana dhambi
akaanza kusifu jinsi nguo zilivyoshonwa kwa ufundi. Akatoka na kurudi kumueleza
mfalme kuwa Abunuwasi kamshonea nguo nzuri sana si za dunia hii kwa jinsi
zilivyo nzuri. Mfalme alifurahi sana, kesho yake akamtuma msaidizi mwingine,
nae kama yule wa jana akarudi kwa mfalme na ripoti nzuri sana ya maendeleo ya
koti, pia akaleta taarifa nzuri kuwa kesho yake Abunuwasi angemaliza kazi na
angeleta nguo ili mfalme azivae. Kesho yake mapema Abunuwasi akaingia katika
kasri la mfalme akiwa kama kashika lundo la nguo, ambazo mwenyewe alisema wasio
na dhambi tu ndio wataziona. Wasaidizi wa mfalme wote hawakuwa wanaona kitu
lakini walianza kupiga makofi wakisifu jinsi nguo zilivyokuwa nzuri, hamna
aliyekuwa anataka kuonekana ana dhambi. Hatimae Abunuwasi akamkabidhi mfalme
nguo, mfalme nae hakuwa anaona kitu lakini ili asiambiwe ana dhambi akajidai
eti nae anaziona akaanza kumsifu Abunuwasi kwa umahiri wake wa kuchagua rangi
na hata ufundi wake mkubwa wa kushona. Abunuwasi akamuomba mfalme azivae zile
nguo, wakaingia faragha mfalme akavua nguo zake na akaanza kuvaa nguo
asizoziona kwa msaada wa Abunuwasi. Kwa vile alivua nguo zote na kuvalishwa
mpya zisizoonekana, rohoni mwake alikuwa anajiona yuko uchi lakini akaona akitangaza
haoni kitu wananchi wangemshangaa kuwa mfalme ana dhambi, hivyo akaendelea
kusifia na kujiangalia kwenye kioo akisifu nguo zilivyompendeza. Kisha
akalazimika kutoka nje ili wananchi waone nguo mpya za mfalme. Wote walikuwa
wanamwona mfalme yuko uchi lakini wakawa wanaogopa kuonekana wana dhambi hivyo
kila mtu akawa anashangilia na kusifu uzuri wa nguo za mfalme. Lakini ghafla
mtoto moja mdogo kwa sauti kubwa akamuuliza baba yake, “Baba mbona mfalme yuko
uchi?”. Minong’ono ikaanza mwishowe watu wakaanza kumuunga mkono mtoto, mfalme
nae sasa aibu ikamshika kwani alijua sasa watu wote wanamuona yuko uchi, akatimka
na kujificha kwenye kasri lake na hadithi yangu imeisha hapo.
Hii imekaa kama vile ni "anti-kutumbua"
ReplyDeleteETI EE
ReplyDelete