12 October 2022

OYAA NIMEJIUNGA NA FREEMASON MSINITAFUTE

Aise juzi niliona tangazo kwenye nguzo ya umeme ya namna ya kujiunga na Freemason. Kulikuwa na namba ya simu ya wakala wa Freemason. Nikampigia, alikuwa jamaa fresh sana , tumeongea nae fresh yaani alikuwa anayajua matatizo yangu utadhani ni ndugu yangu. Hawa jamaa ma Freemason wana uwezo sana aise. Alinieleza masharti ya kujiunga, nikatumia shilingi laki mbili unusu ili aniunge, kanitumia meseji imetoka Marekani tena ya Kingleza imesema Conglations umejiunga na Freemason you will be rich man. Kwa kweli ndoto zangu zote najua zitatimia. Lazima na mimi niwe na demu bomba aliyejichubua na kuwa na makalio ya Uturuki, halafu niwe na gari kali na nyumba ya ghorofa maana yote haya nimeambiwa nikifuata vizuri masharti lazima nitayapata.
 Wiki iliyopita nimepeleka shiling alfu hamsini ambazo zimetumwa Canada ili 
 kunisafisha nyota. 
Unajua mwaka juzi ulikuwa mgumu sana nilitengeneza nyimbo zangu kumi zote hazikuhiti, ndio jamaa yangu mmoja ambaye alikuwa na singo inafanya vizuri akaniunganisha na mganga wake. Mganga akacheki kwanini nyimbo zangu hazihiti, akakuta kumbe kuna wasanii watatu wameshirikiana na prodyusa wangu wameniwekea mkaa kwenye nyota yangu. Mganga akanisaidia kidogo akanambia nilete kuku mweupe na kuku mwekundu kutengenezea dawa ya kusafisha mikosi niliyotupiwa, akanambia nimlipe nusu tu ya fedha yaani shilingi alfu hamsini na nyingine ntamalizia ntakapokuwa supastaa. Nilikamilisha masharti likiwemo kubwa moja kuwa kila nikimaliza kurekodi master niipeleke makaburini kwanza ndio niipeleke redio, alisema hiyo ina maana mizimu isikilize singo yangu kwanza kabla ya watu wengine. Masharti yote nilifwata, nimetengeneza singo sita, singeli mbili, bongofleva mbili, na muziki wa enjili nyimbo mbili, hata moja haipigwi, nimesha honga madj kibao, samahani nimeshawapa madj kibao hela ya promo, bado nyimbo zangu hazipigwi, ni wazi kama gundu nililowekewa ni babu kubwa. We fikiria katika miaka miwili nimetoa singo kumi na sita hata moja haikuhiti si lazima kuna mkono wa mtu hapo? Sasa nimeona hakuna mabadiliko ndio nimeona sasa nijiunge na Freemason. Najua mwaka kesho utanikuta mimi ni superstar.......natafuta hela kidogo za kulipa ili nipate pete ya u Freemason hapo ndio ntakuwa nimejiunga kamili  na ndipo kila  kitu kitakuwa changu. Ngoja nikatafute hela nimalize deni msinitafute...........

24 January 2018

NAMBA YA BABU UNAEMPIGIA HAIPATIKANI

Toka nilipokuwa mdogo nilikuwa naambiwa na wakubwa, ‘Usimcheke mwenzio akipata tatizo’, kiukweli nimekuwa najitahidi sana kufwata ushauri huo, lakini mara nyingine bwana nimekuwa nashindwa kujizuia kuna matatizo mengine yanachekesha  mno. Yaani kama ni rafiki yako kaja kukuhadithia, ingawa anatoka machozi, we unamsikiliza kwa makini halafu unamwambia unaenda bafuni ukifika huko unacheka halafu unarudi na sura flani siriaz, kisha unaendelea kumpa pole.  Sasa ngojeni niwambieni kisa fulani kimemtokea rafiki yangu  mmoja mjanjamjanja wiki iliyopita, yaani bado nacheka japo jamaa yangu akitokeza ghafla nakuwa siriaz, akijua namcheka patakuwa padogo nakwambia.

Huyu jamaa yangu ana tatizo moja kubwa sana, yaani kama vile haamini kuna Mungu, akiamka hana hela basi ataenda kwa mganga akaangalie nani kasababisha mkosi wa namna ile , akipata pesa lazima aende kwa mganga amtengeneze ili wabaya wasije wakazikwapua zile pesa kimiujiza. Akitaka kusafiri lazima akaague, akitaka kupata mpenzi mpya lazima aende kwa mganga, mimi nimeshamsema nimechoka. Najua lazima kishaenda kunicheki kwa wataalamu wake kama mimi nampenda au fiksi hilo nina hakika. Sasa  siku chache zilizopita akapata mesej ndefu kwenye simu yake, meseji ilionekana kama imekosea namba, ilionekana kama meseji imetoka kwa babu mmoja inaenda kwa mjukuu wake. ‘Mjukuu wangu hebu muulize rafiki yako kwanini hanilipi pesa yangu? Mimi nimemsaidia nimempa yule jini mpole kwa laki tano tu na ameweza kwa muda mfupi kumpa mabasi matatu na nyumba nne, sasa kwanini hanilipi? Mwambie zile nyumba zinaweza zote kupukutika, mkumbushe alipe deni upesi niishukuru mizimu’. Nakwambia  jamaa akaja kwangu macho yamemtoka, bila hodi wala salamu akaanza,’Bradha Mungu kanikumbuka, yaani kuna meseji ilikuwa iende kwa mtu mwingine imekuja kwangu na hii ndio itanitoa kwenye umasikini’. Basi akaanza kunisomea ujumbe ule, mi nikamuuliza sasa wewe unahusika vipi hapo? Akacheka kwa dharau na kunambia kuwa mie akili yangu iko sloo sana, akaniuliza kwa dharau ‘Hivi hujui hapa nimeshapata namba ya huyu babu?, kwa hiyo na mimi namtafuta ili anipatie na mimi langu jini nitajirike’. Duh kifupi nilijaribu kila njia kumkanya hakusikia. Sasa  toka juzi ananinisumbua huku analia machozi, eti aliwasiliana na yule babu vizuri, akaambiwa atume laki tatu za kufanyia kafala, baada ya kutuma tu pesa ile namba ya babu haiku tena hewani. Sasa jamani kwanini nisicheke?

11 January 2018

HATA MIMI LEO NDIO MARA YA KWANZA KUMPASUA MTU

Dokta kaingia chumba cha mgonjwa anaesubiri kwenda kufanyiwa operesheni,
DOKTA: Vipi mbona unaonekana umepanik sana?
MGONJWA: Kwa kweli sina raha hii ndio operesheni yangu ya  kwanza, naogopa sana
DOKTA: Usiogope bwana, mi mwenyewe pasonalii ndio ntakae kufanyia hiyo operesheni.
MGONJWA: Loh nashukuru sana, Dokta umeshawahi kufanya operesheni kama hii?
DOKTA: Hapana leo ndio mara yangu ya kwanza kumpasua mtu, lakini usihofu, chuoni nilikuwa napasi sana mitihani

10 January 2018

TUTOTO TWA SIKU HIZI TUKOROFI SANA

Kila mtu anapenda watoto wachanga. Hata jitu ambalo huwa mara nyingi halicheki na mtu liko siriaz wakati wote likikutana na katoto kachanga utakuta linaanza kutabasamu, tena likikabeba katoto kachanga utaona nalo linageuka kuwa litoto. Utaona linaanza kuongea na katoto kachanga lugha za ajabu kabisa utadhani wanaelewana, utasikia, ‘Shum Babu toto shum babu, au shum bibi, shum antii aijigijigijigi, awawawawa, abububujijiji’ na maneno mengine yasiyoeleweka eti ndio mtoto atacheka. Leo niwape siri, mnajua kwanini vitoto huwa vinacheka sana? Vitoto vichanga vimezaliwa na akili sana, sasa huwa vinacheka kuona baba zima au mama zima halijui kuongea vizuri, kitoto kinajisemea moyoni, ‘Huyu mkubwa mzima badala ya kuongea mambo ya maana eti anasema abujibujibujibuji’ kimsingi watoto wachanga wanawacheka sana, muwe mnaongea nao kikawaida, sawa ndugu zangu?
Leo niwape ushauri wababa wenzangu kuhusu taratibu  mbalimbali za kufwata kabala ya kucheza na watoto wachanga, kama nilivyosema vitoto vichanga vina akili sana,  hivyo basi sio kuanza kuvibeba kabla ya kujitayarisha. Najua wabishi wameshakaa mkao wa kubisha, lazima saa hizi wanasema kimoyomoyo,’ Hakuna kitu kama hicho, watoto ni malaika’. Mi nasema sawa hebu nisikilizeni kwanza. Wababa wenzangu, sharti la kwanza usicheze na mtoto mchanga ambaye ndio kwanza katoka kunyonya wakati umevaa shati la au koti lako la bei mbaya, hakikisha imeshapita japo nusu saa tangu amenyonya ndipo uanze kumrusharusha. Watoto hawa wajanja sana, wakijua kuwa umevaa kitu cha bei mbaya  watakutaim na kutumia nafasi hiyo kukucheulia maziwa na kama hukujiangalia vizuri unaweza ukaingia kwenye daladala na michirizi  ya maziwa ya mgando mgongoni.
Sharti la pili linahusu wale ambao hupenda kucheza na watoto kwa kuwanyanyua juu ya vichwa yao, kabla hujaanza kamchezo hako, hakikisha mtoto kavaa nepi. Katoto kakijua una kamchezo hako, katajifanya kanacheka sana na kufurahi kila ukikanyanyua juu, kumbe huo mtego, iko siku ukikanyanyua juu kama hakana nepi katakutaimu na kukukuharishia kichwani, chunga sana, maana inawezekana wakati huo mdomo wako uko wazi. Hutu tutoto twa siku hizi tunaanzaga ukorofi tumboni.


19 December 2017

MBILI KUJUMLISHA MBILI NI NGAPI?

Jana usiku nilisikia mazungumzo haya kutoka kituo kimoja cha redio fm,
MTANGAZAJI: Asante kwa kutupigia simu umepata bahati ya kuingia kwenye shindano letu la zawadi kubwa ya Krismas, uko tayari?
MSIKILIZAJI: Niko tayari
MTANGAZAJI: Swali lenyewe ni la hesabu
MSIKILIZAJI: Mimi mwenyewe mhasibu wa muda mrefu
MTANGAZAJI: Ukitoa jibu sahihi kwa swali hili utapata zawadi yetu nono ya kutembelea pori la Kibiti kwa wiki nzima na kuona uoto asili wa aina mbalimbali unaopatikana katika pori hilo. Hii ni kampeni ya kituo chetu ya kuhamasisha utalii wa ndani. Sasa swali….2 +2 ni ngapi?

MSIKILIZAJI: Saba

13 December 2017

WATOTO WA SIKU HIZI WANAANZA MAISHA NA STRESS

Wakati wa utoto wetu ilikuwa raha sana, unaamka asubuhi unakuta chai au uji unakunywa tena kama hakuna andazi au mkate unalilia mpaka upatikane , ukisha kunywa unatoka nje kwenda kucheza na wenzio mpaka wakati ukiitwa kwa ajili ya chakula cha mchana. Hata usipoitwa njaa ikianza kuuma unarudi nyumbani na kudai chakula, kimetoka wapi, nani kapika hayakuhusu.  Hakuna stress. Lakini siku hizi kuna wazazi wanawapa watoto wao stress mpaka unawashangaa. Kisingizio kikiwa eti ndio maendeleo. Hebu fikiria siku hizi watoto wanaosoma nasari nao wanapewa homwek, jamani muwe na huruma, mtoto akirudi toka shule badala ya kwenda kucheza na wenzie anajipinda kufanya homwek, waalimu na wazazi wanagangamala kabisa wanamwambia mtoto hakuna kucheza mpaka umalize homwek, na mtoto masikini anajipinda maana anajua asipomaliza atakuwa na adhabu shuleni kesho yake. Mtoto anaanza maisha na stress, tumeiga wapi sijui maana hata wazungu wenyewe walioanzisha nasari hawawapi watoto wao homwek. Mtoto anakuwa hajui hata namna ya kujichanganya na wenzie na ndio maisha yake yote anakuwa mtu wa aina hiyo. Utoto wetu kulikuwa na stress moja tu. Siku mama yako atakapoamua kukutuma gengeni utasikia ‘ We Joni, hebu nenda hapo gengeni kanunue mchicha, ukikuta  wanauza fungu shilingi hamsini nunua, kama wanauza fungu shilingi mia usinunue, nunua matembele, lakini kama matembele wanauza fungu shilingi mia, basi nunua kisamvu cha shilingi hamsini, lakini kama kisamvu nacho wanauza shilingi mia , basi nunua mchicha wa mia’ Ukishapata maelezo hayo unakimbia haraka uwaho kurudi utimize amri uende kucheza, lakini ukifika gengeni umechanganyikiwa wala hukumbuki ni nini hasa ulitumwa, kama  ni mchicha au matembele au kisamvu, hapo ndipo stress ya utoto inapoanza ukifikiria kitakachokukuta ukirudi na kuulizia upya, “Eti mama ulinituma nini?” Hizo ndizo stress za utoto. Na stress nyingine kubwa ilikuwa pale unaposhtuka asubuhi na kukuta umekojoa kitandani, hapo inalazimika ubaki kitandani , umejifunika na shuka gubigubi mawazo yote kwenye kipigo kinachokusubiri

5 December 2017

NITUMIE KWA EATELI MANE

KUNA mdada nilikuwa nimemuuzia simu, akalipa nusu, hiyo nusu iliyobaki ikawa tabu kulipa baadae kila nikipiga simu hapokei. Nikaona nimuandikie meseji, 
‘Aise sikuwa na kudai, nilitaka kukwambia  nilikuwa napita huku Sinza mori  nikamkuta msichana mmoja ambaye boyfriend wako alimnunuliaga  simu toka kwangu anapigana na mwenzie, eti  wanamgombea bwana wako. Huyu aliyenunuliwa simu kakong’otwa akakimbilia kwenye gari la boyfriend wako wakasepa’. Haikupita nusu dakika simu ikaanza kuita sikupokea. Baada ya missed call 13, ikaingia meseji, ‘’Wamepigania wapi? Halafu walielekea wapi? Nambie tafadhali tafadhali hapa nataka kufa”. Nikaminya nywiiii shenz taip. Ikaja meseji nyingine, ‘Hela zako ninazo tukutane wapi nikupe unihadithie?’ Nikajibu nitumie kwa eatel mane, niite uber nikupitie nikupeleke anakokaa huyo mdada, mie napajua'. Nusu dakika baadae mkwanja ukaingia, nikazima simu. Mpaka sasa nimelala feni linanipuliza taratibu.


MAPENZI YAMTESA WAKUNYUMBA

HABALI ZA KUNYUMBA, NAITWA KOMBA WA SONGEA, MJOMBA WAKE GULO WA CHINA MJINI, NILIWAHI KUMPENDA DADA MMOJA ANAITWA FALIDA MBAWALA WA BOMBAMBILI , KILA NIKIPANGA KUMWAMBIA NAKUA MWOGA NASHINDWA, SIKU MOJA NIKASEMA NAJIKAZA HADI NIMWAMBIE, ILE NIMEFIKA KALIBU YAKE NILITETEMEKA HADI JASHO NA HIVYO SIKUWEZA KUMWAMBIA,NIKAAMUA KUTUMIA SMS KUMJULISHA HILO, NIKAMWANDIKIA HIVI, "FALIDA NAKUPENDA SAAANA VIPI WEWE JE? NAOMBA JIBU TAFAZALI" MUDA SI MREFU NIKASIKIA SMS IMEINGIA KWENYE SIM YANGU, NIKAWA NATAMANI KUJUA FALIDA AMENIJIBU NINI ILA NIKAWA NAOGOPA KUFUNGUA ILE SMS, NIKASEMA NTAIFUNGUA KESHO, NILILALA KWA TABU SANA USIKU HUO NIKISUBIRI KUJA KUFUNGUA SMS YA MAJIBU YANGU TOKA KWA FALIDA, JAPO NILIWAZA KAMA KANIKATALIA ITAKUWAJE,? ASUBUHI IKAFIKA NIKAFANYA MAMBO YANGU NA ILIPOFIKA SAA NNE ASUBUHI NIKAOGA HALAFU NIKAPANDA KITANDANI NISOME MAJIBU YANGU NA NILIFUNGUA SMS HUKU MAPIGO YA MOYO YAKIWA YANAENDA MBIO, HUKU NAIANGALIA KWA MBALI, NIKAKUTA SMS HII,,'HAUNA SALIO LA KUTOSHA KUTUMA MESEJI HII TAFADHALI ONGEZA SALIO''

23 November 2017

MTANI KALA KASHATA ZA KUNGU 20

MTANI wangu sasa amevuka mpaka, yaani kila nikimkumbuka nacheka mpaka ninashindwa kupumua. Niko na mtani wangu hapa kwenye kidispensari mtaani kwetu  watu wote wananishangaa kwanini namcheka mgonjwa. Ngojeni niwape stori nzima Unajua mtani kaja kunitembelea mjini ili asafishe macho. Alinipigia simu kuwa anataka akirudi kijijini awe na stori za kuhadithia. Kwlei alipofika nimemzungusha sehemu nyingi za muhimu. Nimesha mpeleka baharini akachota maji ya bahari kayaweka kwenye chupa atarudi nayo kijijini kwao, nimeshampeleka kuliona daraja la Kigamboni, na nimepeleka klabu mara mbili. Nimemuingiza kwenye lifti akapanda mpaka ghorofa ya kumi, nimempandisha kwenye ngazi zinazotembea, ameanza kuwa mjanjamjanja. Kama siku tatu zilizopita nikampeleka kula kwa mama ntilie yule wa Kijitonyama ambae ni bingwa wa pilipili kali. Mtani wangu alikula biriani kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kusifia sana wali wa rangirangi kama alivyokuwa akiuuita mwenyewe. Sasa jana mtani kaenda peke yake kwa mama ntilie, baada ya kula wali wa rangi rangi, akaona kashata za rangi nzuri akazitamani, akaulizia bei alipoambiwa akanunua kashata ishirini akafungiwa na kurudi nazo nyumbani. Mtani wangu akazificha vizuri kashata zile  na kuanza kudokoa moja moja akawa anatafuna kwa siri. Haikuchukua muda akamaliza kashata zote.  Niliporudi nyumbani nimemkuta mtani kalala kwenye mkeka nje ya nyumba, nikashangaa maana sio tabia yake, baada ya kumuamsha aliamka lakini akawa amelegea sana, hata macho yake yalikuwa yamelegea kama vile kalewa. Nikadhani labda malaria nikamuuliza kama anaumwa akaninijibu kwa sauti ya kinyonge kuwa haumwi kachoka tu. Kiukweli nikawa na wasiwasi, dalili zote zilionyesha hakuwa salama. Na ni wakati huohuo alipoanza kutimka kukimbilia chooni, ikawa kila dakika tatu anarudi chooni, anadai tumbo limechafuka namuuliza alikula nini hajibu. Ila alikuwa anazidi kulegea nikaona asije akanifia ndugu zake wakanila nyama, ndio nikamleta hapa dispensary. Dokta kamuuliza mtani wangu alichokula ndipo kwa aibu akalazimika kueleza kuwa alinunua kashata nyingi na amekula zote. Mi nikamuuliza alinunua wapi zile kashata, akajibu kule kwa mama ntilie wa Kijitonyama, hapo ndipo nilipoanza kucheka karibu nivunje mbavu. Ni kweli mama ntilie wa Kijitonyama anatengeneza kashata, lakini kashata zake si za nazi na wateja wake ni wanawake tu maana kashata zake ni za kungu. Ndio maana mtani macho yamemlegea, kafakamaia kashata 20 za kungu dahh 
MTANI wangu sasa amevuka mpaka, yaani kila nikimkumbuka nacheka mpaka ninashindwa kupumua. Niko na mtani wangu hapa kwenye kidispensari mtaani kwetu  watu wote wananishangaa kwanini namcheka mgonjwa. Ngojeni niwape stori nzima Unajua mtani kaja kunitembelea mjini ili asafishe macho. Alinipigia simu kuwa anataka akirudi kijijini awe na stori za kuhadithia. Kwlei alipofika nimemzungusha sehemu nyingi za muhimu. Nimesha mpeleka baharini akachota maji ya bahari kayaweka kwenye chupa atarudi nayo kijijini kwao, nimeshampeleka kuliona daraja la Kigamboni, na nimepeleka klabu mara mbili. Nimemuingiza kwenye lifti akapanda mpaka ghorofa ya kumi, nimempandisha kwenye ngazi zinazotembea, ameanza kuwa mjanjamjanja. Kama siku tatu zilizopita nikampeleka kula kwa mama ntilie yule wa Kijitonyama ambae ni bingwa wa pilipili kali. Mtani wangu alikula biriani kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kusifia sana wali wa rangirangi kama alivyokuwa akiuuita mwenyewe. Sasa jana mtani kaenda peke yake kwa mama ntilie, baada ya kula wali wa rangi rangi, akaona kashata za rangi nzuri akazitamani, akaulizia bei alipoambiwa akanunua kashata ishirini akafungiwa na kurudi nazo nyumbani. Mtani wangu akazificha vizuri kashata zile  na kuanza kudokoa moja moja akawa anatafuna kwa siri. Haikuchukua muda akamaliza kashata zote.  Niliporudi nyumbani nimemkuta mtani kalala kwenye mkeka nje ya nyumba, nikashangaa maana sio tabia yake, baada ya kumuamsha aliamka lakini akawa amelegea sana, hata macho yake yalikuwa yamelegea kama vile kalewa. Nikadhani labda malaria nikamuuliza kama anaumwa akaninijibu kwa sauti ya kinyonge kuwa haumwi kachoka tu. Kiukweli nikawa na wasiwasi, dalili zote zilionyesha hakuwa salama. Na ni wakati huohuo alipoanza kutimka kukimbilia chooni, ikawa kila dakika tatu anarudi chooni, anadai tumbo limechafuka namuuliza alikula nini hajibu. Ila alikuwa anazidi kulegea nikaona asije akanifia ndugu zake wakanila nyama, ndio nikamleta hapa dispensary. Dokta kamuuliza mtani wangu alichokula ndipo kwa aibu akalazimika kueleza kuwa alinunua kashata nyingi na amekula zote. Mi nikamuuliza alinunua wapi zile kashata, akajibu kule kwa mama ntilie wa Kijitonyama, hapo ndipo nilipoanza kucheka karibu nivunje mbavu. Ni kweli mama ntilie wa Kijitonyama anatengeneza kashata, lakini kashata zake si za nazi na wateja wake ni wanawake tu maana kashata zake ni za kungu. Ndio maana mtani macho yamemlegea, kafakamaia kashata 20 za kungu dahh 

15 November 2017

WAHENGA WENZANGU TUHAME MJI MAPEMA

Ndugu wahenga wenzangu, salama macho? Ndege itatua au fitna? Basi tutayafiksi au vipi? Basi doleeee na baada ya salamu naomba niwaambie wazi kuwa hofu nyingi na mashaka juu yenu mliye mbali na upeo wa macho yangu mhenga mwenzenu. Ndugu wahenga, samahani natumia neno ndugu, si mnakumbuka enzi zetu kila mtu alikuwa anaitwa ndugu, tulikuwa hatuitani sijui, oyaa, mshkaji, mkuu, kibosile, mheshimiwa, mtukufu, sisi wote tulikuwa tunaitana ndugu, kwa hiyo ndugu wahenga mambo yamekuwa si mambo tena, sisi wenyewe ndio tulisema ‘asiyekubali kushindwa si mshindani’. Ndugu zangu tukubali tumeshindwa na nashauri tuhame mji tuwaachie wenyewe. Wahenga mambo yamebadilika juu chini, enzi zetu mnakumbuka binti akipata mimba nje ya ndoa alikuwa akijificha kwa aibu na mara nyingine aliweza hata kunywa sumu? Siku hizi binti akipata mimba nje ya ndoa ndio kwanza anapiga picha tumbo analiweka mtandaoni dunia nzima ilione, hajali kama ataliona baba mkwe wake wala baba yake mzazi, yaani we acha tu. Ndugu wahenga mtakumbuka kitu hicho kingetokea enzi zetu mwaka huo hata mvua isingenyesha hapo kijijini na mizimu ingetoa adhabu hapohapo, pengine ukoo wa binti aliyefanya kufuru hiyo ungefukuzwa wote kijijini, a pagelazimika kufaya tambiko la kuchinja ng'ombe dume wawili. 
Siku hizi unaweza kuona mama yake mzazi akisifia kitendo hicho, na kushukuru Mugu kwa binti yake kuwa mjamzito hapo uaanza kusukwa mtego ili aliyempa mimba atolewe upepo, wala sio lazima amuoe, kikubwa aaze kuleta pesa za matunzo.
 Ndugu wahenga mnakumbuka zamani binti wakati anaolewa alikuwa mtu wa aibu tena na machozi yatamtoka kwa uchungu wa kuachana na familia yake? Siku hizi kuolewa kunafanyiwa utani tu, wala wazazi hawataarifiwi, bibi harusi anaruka ruka harusini kuliko hata bwana harusi, yaai mambo yamegeuka uaweza kukuta bwana harusi ndie katulia aaonekana kuwa a mawazo ya jinsi ya kuanza maisha na bibi harusi mapepe.
 Ndugu wahenga mnakumbuka tulivyokuwa tunapishana kistaarabu barabarani wakati tukiendesha baiskeli zetu za foneksi a raleee na magari yakipita barabara hiyohiyo, jaribu leo kupita na baiskeli yako, utagongwa na bajaj, ezi zetu (tunaziita pikipiki za magurudumu matatu) au gari au bodaboda (tulikuwa tuaziita tukutuku au pikipiki) kabla hujafika mbali, na watu wote watakujia juu kwanini unaendesha baiskeli barabarai, sasa baiskeli iaedeshwa shambani?
 Ndugu zangu wahenga, enzi zetu za redio tulikuwa tukisikiliza maneno ya busara na muziki wenye burudani na mafunzo kutoka kwenye redio lakini sasa usishangae matusi ya nguoni yakitajwa na kuambia ndio muziki, na huko kwenye luninga hakuna afadhali, picha  zinaonyesha wajukuu zetu wakijitahidi kushindana kuvaa nguo ndogo zaidi kila siku, eti ndio wimbo utapendwa.
Ndugu zangu wahenga nawaomba tuwaachie hawa mji, tutafute mji mpya huko porini tuanze moja, tuwaachie waendelee kudaiana fidia ya matunzo ya watoto ya mamilioni kwa mwezi. Tuwaachie watoto wa kiume waendelee kuvaa suruali zinazolegezwa makusudi ili makalio yaonekane, sijui ili nani awaone? Tuwaachie mji mabinti wanaojifanya wanaume. Ndugu wahenga tuhame mji, iko siku hawa watatuhamisha kwa nguvu tukubali tumeshashindwa…. 

11 November 2017

PILIPILI YA MAMA NTILIE KIJITONYAMA ILITAKA KUNITIA UCHIZI

Unajua  kuna mama ntilie mmoja pale mitaa ya Kijitonyama lazima sasa niongelee ishu zake. Mdada huyu mpishi mkali sana, wali maji, wali nazi, pilau, biriani, uji wa mchele vyote hivyo ukitaka utapata, bila kusahau ugali wa muhogo, ugali wa sembe halafu alivyo na utaalamu ndie peke yake mjini hapa anaeweza kupika ugali wa ngano, najua wabishi mtaanza ohh toka lini kukaweko na ugali wa ngano? Nyie nendeni pale Kijitonyama.

Achana na ugali wa ngano, huyu mdada ishu kubwa kuliko yote ni pilipili yake. Jamani kama duniani kuna kiungo kinachoweza  kuleta apetait sana, yaani kinaweza kukufanya uwe na hamu ya kula chakula kingi zaidi, kiungo hicho kinaitwa pilipili. Huyu mdada wa Kijitonyama anatengeneza mwenyewe pilipili yake, sijui anatengenezaje pilipili hiyo maana nilishakutana na pilipili kali lakini  huyu mdada pilipili yake  ni zaidi kali. Ukitaka kutumia pilipili yake lazima ujitayarishe kisaikolojia. Ukijitia kukumia bila matayarisho unaweza kutamani kukata ulimi laiv. Yalinikuta juzi nikaagiza biriani nikawekewa na pilipili pembeni , haraka nikasambaza pilipili kwenye biriani yote. Nikachota kijiko kikubwa kilichojaa biriani nikaweka mdomoni, ilichukua kama sekunde ishirini kwa akili kupata habari kuwa kwenye ulimi kuna moto unawaka. Bila kuanza kudadisi, akili ikatoa amri fasta kuwa lazima kutema hiyo biriani . Kulikuwa na jamaa mwingine jirani yangu ambaye naomba nichukue nafasi hii kumuomba radhi kwani nilimuogesha ile biriani kutoka mdomoni. Nilijaribu kuangalia maji yaliyokuweko jirani ninywe nipunguze moto mdomoni,  jicho liliangukia kwenye maji ambayo muda mchache uliopita wateja tulinawa, hilo halikunisumbua, haraka sana niliyagugumia, lakini wapi ulimi uliendelea kuwaka moto, machozi yalikuwa yanatiririka bila aibu, nikakimbilia bomba la maji jirani kulifungua hakikutoka kitu, kumbe maji yalishakatwa siku nyingi, ikabidi ninywe tu maji waliyotumia kuosha viazi yaliyokuwa kwenye ndoo moja ya plastiki. Kiukweli sitasahau maana nilitimka kukimbilia duka la jirani nikanunua soda mbili baada ya kumaliza ndipo kidogo nikaanza kuona nafuu, akili ikaanza kurudi. Pilipili ile huwa inanijia mpaka kwenye ndoto, kuna siku nikaota nimeila tena nilizinduka usingizini na kukimbilia maji. 

25 October 2017

CHEZA na mtu mwingine lakini usicheze na Mbongo.

 Yaani Mbongo ana njia mbadala nyingi za kubadili tatizo kuwa fursa. Hizi wiki chache zilizopita nimekuwa najitahidi kuhudhuria harusi ili nijifunze ubunifu wa Wabongo, nakwambia si mchezo hawa jamaa waone hivi hivi. Baada ya kuingiza kipengele cha hotuba za wazazi, ambapo wazazi husimama na kutoa hotuba ndefu nyingine zinaboa vibaya sana nikawa najiuliza kwanini ma emsi wasifute hiki kipengele, kinapoteza muda tu, we jitu zima linaolewa ndio unadhani hotuba za siku ya harusi zitabadilisha tabia ya mtu? Yaani hapo ni siasa tu. Si unajua wanasaisa wanavyohutubia  mambo hata hawayajui, we utakuta mtu akichaguliwa tu na wananchi basi anajiona anajua kila kitu, utasikia anatoa ushauri wa kilimo, ujenzi, ufugaji, usanii kila kitu anajua. Ene wei hao ndio kazi yao turudi harusini, niliongea na Emsi mmoja akanambia kumbe vile vipengele ni njia mbalimbali za kupoteza muda watu wasiombe vinywaji, hasa wale waliochanga, ni changa la macho kuonyesha shughuli ilikuwa na vipengele vingi ili muda haukutosha.

Sasa siku hizi kuna kipengele kipya. Maharusi siku hizi wanakuwa ndio wasanii watumbuizaji kwenye harusi yao wenyewe. Yaani michango ikionekana imekaa vibaya maharusi wanataarifiwa waanze mazoezi ya kucheza na kuimba ili kupunguza gharama ya kukodi wasanii. Basi hapo utamkuta bwana harusi bizi anafanya mazoezi kuimba na kucheza kama Ali Kiba au Daimondi, mwezi mzima maharusi wanakaa mbele ya TV wanaangalia video za Kinaijeria za akina Davido wajifunze namna ya kucheza, wengine ambao kidogo Kingleza kinapanda wataanza kufanya mazoezi ya wimbo wa Endless love. Basi siku ya harusi kipengele cha wasanii watumbuizaji wanakibeba wao wenyewe. Ile kuingia ukumbini, wanacheza nusu saa pale mlangoni, kuimba wimbo wa pamoja nusu saa, Emsi kuwasifu kwa usanii nusu saa, inakuja hotuba ya baba mzazi wa mume nusu saa , mama mzazi wa mke nusu saa, ujue hapo saa nne usiku imeshaingia, chakula kinaletwa watu wanakula mpaka saa tano, bwana na bibi harusi wanaimba tena, unasikia jamani wenye ukumbi wameruhusu mpaka saa sita tu hivyo sherehe imeishia hapa. Milioni salasini mliochanga ndio imeisha hivyo mjue.