19 October 2017

USHAURI MUHIMU KWA WANAUME WA BONGO;


UKIWA  na bebi wako halafu akaguna ghafla na kusema neno 'Yaaani'. Chonde chonde usikosee ukauliza ' Vipi baby?'. Huo ni mtego wa pesa. Hapo jibu lake ni matatizo lukuki ambayo ukishayajua utakuwa umekwisha ingia kwenye mtego wa kuyalipa. Hivyo ukimsikia bebi wako ghafla, kasema ' Mhhh yaani', we jifanye hujasikia endelea na shughuli zako au mpe  busu jingine la haraka haraka kabla hajasema neno jingine
 By Muathirika

BAHATI NZURI UTUMBO WOTE NIMERUDISHA NDANI




Jamaa fulani alikuwa na tabia ya kutoa ushuuz kwa nguvu kila aamkapo asubuhi. Mkewe alikerwa sana na tabia hiyo, alimkataza akachoka, siku moja akamwonya kuwa iko siku badala ya ushuzi, utumbo utakuja kumtoka. Jamaa alicheka sana kusikia hilo. Siku moja mke alilazimika kuamka alfajiri awatengeze kuku kwa ajili ya sherehe, alipowatoa utumbo wale kuku akakumbuka alichowahi kumwambia mumewe akaamua kumtisha, akamnyatia mumewe ambaye alikuwa bado amelala na kumuwekea utumbo kwenye pajama lake na kurudi jikoni. Muda si mrefu mwanaume aliamka akaachia ushuzi kwa nguvu kama kawaida yake, lakini akahisi kitu cha baridi ndani ya suruali, ile kuvuta si akakuta utumbo. Akapiga ukelele,’Mama yangu nimekufa’. Mke wake aliposikia akacheka peke yake, akajua jamaa kashaukuta ule utumbo. Kimya cha kama nusu saa kilipita. Hatimaye jamaa akamfuata mkewe jikoni akiwa amelowa jasho pajama nzima.

JAMAA: Mke wangu yale uliosema leo yametokea.

MKE: Yepi jamani?

JAMAA: Mke wangu ulisema nikiendelea kujamba utumbo utatoka, leo utumbo si umetoka kama ulivyosema

MKE: Pole mume wangu, sasa imekuwaje?

JAMAA: Namshukuru Mungu, nimejitahidi nimeusindilia na vidole na nimeweza kuurudisha ndani wote.

MKE: Mungu wangu umefanyaje wewe?


WALEVI WAKO LEVO NYINGINE

Naishi karibu na baa moja maarufu, kwa hiyo kila siku naona vituko vya walevi na kushukuru kuwa mimi sio mmoja wao. Walevi bwana wanavituko japo wenyewe hawajui kuwa ni vituko, na ukitaka ugomvi nao waambie kuwa wanavituko. Najua hata sasa mlevi akianza kusoma tu hii habari atachana hili gazeti, ndio zao. Kitu cha kwanza mlevi hakubali kuwa yeye ni mlevi, atakwambia yeye ni mnywaji, pamoja na kuwa hata anachokunywa kimeandikwa kuwa ni kilevi bado atakubishia kuwa yeye si mlevi. Walevi wako wa aina nyingi sana, lakini kimsingi pombe humfanya mtu ajione yeye yuko tofauti na kawaida. Hivyo mtu ambaye hajui Kiingereza akilewa anajiona anajua sana lugha hiyo, na hivyo usishangae akianza kusisitiza kuongea Kiingereza japo hajui. Kwa msingi huohuo, wako wale ambao wanajijua hawana uwezo wa kupigana lakini akilewa anajiona anauwezo wa kumpiga kirahisi Meiweza na hivyo walevi wa aina hii huwa wanapenda sana kuanzisha ugomvi, ili wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Shida inakuja wakati mlevi anapojiona kuwa yeye ni mwalimu wa kung fu, nyie wote mnamuonea huruma hata kusimamama hawezi wakati yeye anajiona anaweza kuwapiga watu wote kung fu kirahisi kama kwenye video. Juzi usiku wa manane polisi wamekuja kuwatimua walevi waliopitiliza muda, mmoja wao akadai amesoma sana sheria na kuanza kutaja vifungu vya sheria vinavyomruhusu binadamu kunywa pombe wakati wowote, na kugoma kupanda karandinga, akaishia kupigwa virungu vya kwenye visigino mwenyewe akapanda gari la polisi. Halafu kuna walevi wadada waliowatoroka wapenzi wao, hawa wanachekesha kweli, wakipigiwa simu kwanza hutimka mbio na simu kukimbia kelele za muziki, wala hawafiki mbali kwa akili zao wanajua muziki hausikiki, utasikia ‘Bebi vipi mbona unapiga simu wakati nimelala?’ Baada ya sekunde utajua tu kuwa aliyeupande wa pili anasikia muziki na ameulizia, mdada mlevi utasikia ‘Huo muziki unatoka nyumba za jirani kuna kigodoro’ Hapo anakuwa kajichanganya maana Zilipendwa ya Chibu inasikika wazi. Ila raha kubwa ni pale mlevi kaishiwa lakini hataki kuondoka kaunta, msikilize anavyotamba kuwa anapesa benki zote za mjini, hapo anadhani eti ndio atakopeshwa kwa mali kauli hiyo.

14 October 2017

NIMESHTAKIWA NAWAHI MAHAKAMANI KABLA HAWAJAFUNGUA MILANGO SIOGOPI

Unajua Mbongo wa kawaida akipata kesi anapaniki, Atajaribu kila njia kumaliza kesi nje ya mahakama, ikishindikana huanza kutafuta ndugu na marafiki wampe ushauri afanye nini? Amuone nani? Hapo ndipo ataliwa pesa na ndugu na rafiki zake na kusitokee msaada wowote. Akistuka basi ataanza kumtafuta polisi aliyeshika kesi, na akiona huku kumeshindikana basi utasikia kagonga hodi kwa mganga na kuomba dawa ya kufuta  kesi, eti kesi yake ifutike kimiujiza, hapo ataliwa tena mkwanja wa nguvu, kuku kadhaa watapoteza maisha na kesi huwa inaendelea, na inaweza ikaishia jamaa akafungwa kirahisi tu. Sasa mimi nina kesi mbili nimeshtakiwa , lakini nasubiri kwa hamu kwenda mahakamani tena nitawahi mimi kabla ya walalamikaji. Kesi zote zinahusu kuharibu mali za watu. Hii ya kwanza ilinikuta pale Mwenge, nilikuwa nimeazima gari la baba mdogo napiga misele si nikajikuta kwenye barabara inayopita katikati ya ilipokuwa stendi ya Mwenge. Kuna jamaa wenye akili za kiajabu ajabu wanabiashara ya kuuza viatu vya mchuchumio, hao wamepanga viatu vyao mpaka barabarani, na wanategemea gari zikwepe viatu vyao. Sasa nilipofika hapo ikawa tupishane na daladala, barabara imekuwa nyembamba, ningekwepa viatu ningepigwa pasi na daladala, nikaona sipendi ujingaujinga, nikavikanyagilia mbali viatu vya mchuchumio vilivyokuwa barabarani. Jamaa wakaanza kelele na vurugu na ndio wamenishtaki  kwa kuharibu mali yao, nimesema nawahi mahakamani kabla yao. Kesi nyingine imenikuta eneo la Shekilango, serikali imetengeneza barabara ya kisasa, ina njia ya watembea kwa miguu na njia ya kwa ajili ya bodaboda na baiskeli. Jamaa wanaojifanya akili zao hazina akili wamepanga bidhaa zao na kuziba njia ya bodaboda na baiskeli, watembea kwa miguu na bodaboda wanalazimika kututumia njia moja. Mi nimepitisha bodaboda yangu katikati ya mali zao walizopanga kwenye njia ya bodaboda, sikuona sababu ya kuwasumbua waenda kwa miguu kwenye njia yao sababu ya wakorofi wachache. Jamaa wamenishtaki nimetangulia mahakamani nawasubiri sipendi ujinga mimi.  

6 October 2017

KUMBE KISIRANI CHANGU KIMO KWENYE DAMU

Unajua binadamu mara nyingi hatujijui uwezo wetu mpaka litokee jambo la kutuamsha. Kwa mfano mtu hujui uwezo wako wa kukimbia mpaka siku ile unapotimuliwa na simba na ndipo hapo utakapogundua huyu mkimbiaji Husaain Bolt hana lolote mbele yako. Au siku ukikalia nyoka kwa bahati mbaya ndipo utajua kumbe unaweza kuruka kisarakasii mita tano kwenda  juu kwa kutumia makalio tu, sio mchezo. Jana tu na mimi nikagundua siri yangu kubwa sana, ngoja niwahadithie. Watu wengi hudai kabila letu ni tabia ya kuwa na hasira kaliJana tu na mimi nikagundua siri yangu kubwa sana. Watu wengi hudai kabila letu lina tabia ya kuwa na hasira kaliJana tu na mimi nikagundua siri yangu kubwa sana. Watu wengi hudai kabila letu ni tabia ya kuwa na hasira kali, tena inadaiwa ukituudhi tunakumaliza kisha tunajinyonga. Kila siku nimekuwa nabishana na watu na kuwaambia kuwa hizo ni hadithi zilizotungwa na watani wetu,au la  kama kweli basi ilikuwa zamani. Jana tu nimegundua ukweli wa ishu hiyo.

Nilipanda daladala moja toka Sinza kwenda Gerezani, unajua safari hiyo ndefu, basi kabla ya kupanda nikanunua gazeti langu la Risasi niwe nasoma njiani. Nikapata kiti, sijajipanga vizuri akaingia jamaa mmoja akakaa pembeni  yangu. Hakuchelewa nikasikia, ‘Bro samahani naomba gazeti nipitishe pitishe macho’. Dah kwa shingo upande nikampa nikijua atapitisha na kunirudishia kabla ya kituo cha pili nifaidi gazeti  langu. Jamaa akanza kusoma kwa makini, hakuacha kitu alikuwa anasoma mpaka namba ya ukurasa, ghafla akapigiwa simu, inaonekana alikuwa anapewa namba ya simu, maana aliniomba peni nikampa, si akaanza kuandika namba anayotajiwa kwenye gazeti langu, akaandika na jina na mtaa aliotajiwa, simu ikaisha akaendelea kusoma gazeti langu na kwa kutumia peni yangu akawa anapigia mistari sehemu zilizokuwa zina mfurahisha. Sasa nikaanza kusikia hasira kwa mbali, hasira ambayo sikujua ninayo, nikawa najiuliza huyu jamaa vipi? Nikamuomba gazeti langu, akajinijibu, ‘Subiri kidogo sijamaliza’. Sikumbuki vizuri nini kilinijia lakini nilijikuta tu nimemlamba kichwa nikamnyang’anya gazeti na kulichanachana  na kutafuna kipande alichoandika namba ya simu. Kisha nikaruka toka kwenye basi wakati bado liko kwenye mwendo.  Leo nimewaza sana nimegundua kuwa ile habari kuhusu kabila letu ni kweli na imo kwenye damu yangu.

BABA KUNA JINI KABATINI

Mzee karudi kazini mwanae mdogo akamuwahi,
DOGO: Baba usiingie ndani kina jini chumbani kwenu
BABA: Hakuna kitu kama hicho
DOGO: Kweli baba kuna jini liko kwenye kabati lenu la nguo....Mzee kaingia ndani kamkuta mkewe kalala kitandani kajifunika shuka gubigubi hadi kichwani. Kaenda kwenye kabati kufungua mlango , akamkuta rafiki yake wa miaka mingi yuko uchi ndani ya kabati

BABA: Aise unajua we fala sana, we rafiki yangu miaka yote hiyo halafu unamtisha mwanangu eti wewe jini, hebu toka huko nenda kwenu kacheze michezo hiyo na mwanao.

30 September 2017

HOTUBA YA MAMA MKWE HALOOOO

Mi nadhani hizi  taratibu za zama zenu hizi za kuruhusu hotuba kutolewa kwenye sherehe za harusi zingeangaliwa upya, turudi kwenye taratibu safi za enzi zetu, ambapo hakukuwa na mambo ya hotuba, mara ya bibi harusi halafu ya bwana harusi, halafu  hotuba za wazazi, siku hizi na wenyeviti wa kamati nao wanaongea, basi vurugu tupu. Au la, hotuba zihakikiwe, mtu atakae taka kuongea aandike kabisa hotuba yake na kuituma kwenye kamati ya harusi ili  ihakikiwe. Nasema hivi kwa kuwa Jumamosi iliyopita nilihudhuria sherehe za harusi kwenye ukumbi wa mji mmoja unaojisifu kwa kuwa ndio chanzo cha mapenzi, baada ya shamra shamra za kila aina zilizokuwa zinaendeshwa na MC mdada mmoja mwenye jina matata sana. Tukatangaziwa kuwa  baba mzazi wa kijana ana machache ya kusema na kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa, baba hakusema sana zaidi ya kumtakia mwanae maisha mema yenye raha. Kisha tukatanganziwa kuwa mama wa bibi harusi anataka kuongea,hapo ndipo vituko vikaanza. Mama mkwe alisindikizwa na akina mama wenzie ambao walikuwa wamevalia Madera mekundu sare, wimbo wa Msagasumu  uliporomoshwa, mama mkwe na kundi lake wakaanza kumwaga razi kwa mauno ya nguvu, nikamuangalia bibi harusi nikakuta anashabikia kwa kupiga makofi na kufurahi alikuwa kama nae anataka kwenda kujiunga na mama yake, wakati bwana harusi alionekana kushangaa vituko vya mzazi wake mpya. Hatimae mama harusi akapewa maik, hapohapo akaanza, ‘Halo halo ya harusiii’ watu wote tukajibu ‘Haloooo’. Mama mkwe akakaa sawa na kuanza kutoa nasaha. ‘ Mwanangu hongera kwa kuolewa, walisema sana mtaani, naona umewaziba midomo wale mashoga zako wasiojua kuoga haloooo. Haya baba, mke ndio huyoo umepata, mwanangu mzuri kama unavyoona, hana kovu mwanangu, labda kama hizo tatuu zake za mgongoni na tumboni utaziita makovu. Mwanangu kalelewa kwa uhuru anapenda starehe, na wewe mlikutana disko nisisikie unaanza kumbana eti asiende disco, mwanangu anapenda ngoma na nimemlea apende utamaduni wake, sasa nisisisikie eti ohh unamfungia ndani asiende kupandisha mzuka ngomani, mwanangu sio dobi, nguo zako peleka kwa dobi, mwanangu sio mpishi wa hotelini hivyo sio kumlazimisha apike  akaja ungua na miuji ya ugali bure hana kovu huyo. Mwanangu kifupi ukiona yanakuzidi, rudi kitanda chako ziuzi wala sigawi, wanaume nawajua mie. Haloooo’

11 September 2017

HOTUBA YA BABA MKWE ILIKUWA YA MWAKA


Yaani baba mkwe katoa mpya juzi, mpaka sasa bado sijajua nicheke au nisikitike, maana nasema tena baba mkwe katoa mpya. Juzi Jumamosi tulifanikisha sherehe ya harusi ya mtoto wa kiume wa rafiki yetu. Sisi ndio tulikuwa wanakamati hivyo kwanza nijisifu tuliwezesha bonge ya harusi, japo huwa nawaza tu ule mkwanja tuliokusanya wangepewa hawa maharusi hakika wangemaliza umasikini na kuanza maisha ya kifahari, lakini ndio hivyo tena tulipanga kutumia mamilioni yote yale kwa ajili ya kula na kunywa kwa masaa machache tu.

Turudi kwa baba mkwe, sherehe ilianza vizuri kabisa, MC alikuwa mmoja wa wale ma MC ambao wanapenda kusikia sauti zao wenyewe basi anaongea huyo, kila jambo analirefusha mpaka inachosha. Hatimae ikafika wakati MC akatutangazia kuwa baba mkwe anataka kuja kutoa wosia. Binafsi kipengele hiki huwa kinanichekesha sana, kama mtoto hakupewa malezi mazuri, haka kahotuba ka dakika za mwisho ndio kweli katarekibisha tabia zao kweli? Tuache hayo, baba mkwe akakamata maik, akasalimu ‘Mambo?’. Hapohapo nikashtuka, nikaona baba mkwe huyu wa kileo sana, baada ya kumcheki vizuri nikagundua kuwa kinywaji alichokuwa amekunywa vimemchangamsha kidogo. Baba mkwe baada ya kujibiwa salamu zake akaanza hotuba ambayo sitaisahau mapema. ‘Kijana upo? Naona umeamua kumuoa binti yangu, mimi kama baba yake nasema wazi inaonekana humfahamu binti yangu vizuri, mtu anaemfahamu binti yangu hawezi kufanya uwenda wazimu wa kutaka kumuoa huyu mtoto’. Dahh ukumbi mzima ugeuka kimyaa, bibi harusi alikuwa kajiinamia. ‘Huyu binti yangu ni mkorofi katusumbua sana mimi na mama yake, toka alipofikisha umri wa miaka kumi na sita. Kafukuzwa shule tatu, kila shule ikilalamika kuwa anawaharibu wanafunzi wenzie. Hatimae shule ikamshinda, kifupi sijui haswa baada ya hapo alikuwa anaishi wapi. Japo mara chache alikuwa analala nyumbani. Huyu binti yangu hebu fikiria hata instagram walifungia ukurasa wake kutokana na picha alizokuwa akiziweka humo. Nadhani kijana ulimuona picha zake kwenye magazeti ukaona umepata malaika, hafai kabisa huyo hafai. Nimeona nikueleze ukweli usije baadae kunilalamikia mashetani yake yakimpanda. Mimi na mama yake sasa tunaondoka, tulikuja kuwaonya tu ili msije kutusumbua baadae, pole kijana wangu’ Baba mkwe, mama mkwe, mashangazi, wajomba, makaka haooo wakasepa.

9 September 2017

ASANTE SANA BWANA HARUSI


Unajua kila zama zina mambo yake , teknolojia nayo inasababaisha kuweko mambo ambayo wazee kama mimi tunabaki kushangaa tu nini kinaendelea. Katika jambo ambalo limefanya mabadiliko makubwa ni eneo la sherehe za harusi. Enzi zetu watu walikuwa wanatafutiwa wachumba, mwanaume unaambiwa kuna binti umetafutiwa lazima ukubali, na mabinti vile vile wanatafutiwa mume na hakuna kubisha, taratibu zote zinafaywa na wazee wewe unakabidhiwa mzigo tu.

Siku hizi ndugu yangu kila harusi inatengeneza vipengele vipya. Zamani bibi harusi na bwana harusi walikuwa ni watazamaji tu wa sherehe yao wenyewe, siku hizi wanashiriki kila kitu ikiwemo kutoa hotuba. Wiki iliyopita niliingia kwenye harusi ambayo bwana harusi alitoa hotuba kali sana. Baada ya MC kututanganzia kuwa bwana harusi ana machache ya kusema  tukaanza kumsikiliza. Akiwa na suti yake maridadi akakohoa kidogo kasha akaanza, ’Asante MC, kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa kumuumba mke wangu, kwa hilo Mungu uko juu. Pili nimshukuru baba mwenye nyumba wangu kwa kukubali niwe na deni la kodi ili kufanikisha harusi hii. Naomba nitoe shukrani kwa bosi wangu kwa kunipa likizo fupi ili nikamilishe shughuli hii. Naishukuru kamati yangu ya harusi kwa kuwezesha kukusanya fedha zilizofanikisha kulipa mahari, nimshukuru mke wa kaka yangu kwa kutuazima gauni la harusi, na kaka yangu kwa kuniazima suti hii niliyovaa. Natoa shukrani kwa mtengeneza keki, leo hakuna kukata keki, nitairudisha keki kwako kesho kama tulivyokubaliana. Nawashukuru wazazi wangu kwa kuja na kikundi cha ngoma toka kijijini, kweli kimeziba pengo la burudani katika harusi hii. Naishukuru kamati ya wazee wa kanisa kwa kufanikisha kumshawishi mke wangu aolewe na mimi, niwape aksante kwa akina mama jirani kwa kuja na vyakula toka makwao ili kufanikisha harusi hii, na vijana kwa kuja na pombe za halali na haramu mradi harusi hii ni furaha tupu. MC wewe ni rafiki yangu nashukuru kwa kukubali tulipane kidogokidogo aksante sana’ Kisha bwana harusi akakaa chini watu wote tukabaki kimyaaaaa


26 August 2017

MJINI KUMEJAA MACHIZI

YAANI hapa mjini ukipaangalia kwa makini unaweza ukajikuta unacheka peke yako barabarani watu wakadhani we chizi kumbe unakumbuka uchizi wa wakazi wa mjini. Yaani kuna vitu watu wanafanya havieleweki, wanajitengenezea mazingira ya kupata matatizo makubwa. Hebu we fikiria, jamaa anakuwa na mabinti 15 kila mmoja anamwambia anampenda kuliko kitu chochote duniani. Wote hao wanamuangalia yeye kwa matumizi yao ya kila siku ili waonekane wa maana mjini, na wote wamemuomba awanunulie simu, wengine Samsung model mpya, wengine iPhone6 na wote amekubali maombi yao, baada ya hapo anaanza kuhangaika kuuza hata mali zake na za kazini kwake ili afurahishe timu yake ya wapenzi. Sasa kwanini nisicheke peke yangu? Wakati huo fala huyu anatakiwa kulipa kodi ya nyumba yake ale vizuri apeleke matumizi kwa wazazi wake, yaani kama sio uchizi huo ni nini? Halafu kuna hawa jamaa ambao wako kibao hapa mjini, utawakuta kila siku baa. Hawa wanaanza siku na kilo mbili za mishkaki na ndizi tatu, kachumbari pembeni, baada ya hapo chupa zinaanza kuteremeshwa na ofa kutolewa kwa marafiki na mashabiki. Na wakati huo zoeezi la kuagiza nyama na supu ya pweza linaendelea tena na tena, kimsingi mpaka jamaa anaamua kuelekea nyumbani kwa mke na watoto wake wane amekwisha tumia kitu kama laki mbili kwa masaa manne. Sasa kwake sasa, watoto wamekula ugali kwa mchicha, tena unga wenyewe ulikuwa hautoshi wamelala na njaa, watoto wamelalia kigodoro cha nchi moja wakishindana kuvutana shuka moja, yeye mwenyewe anapokuja kulala ni juu ya godoro limechoka kabisa anajifunika kanga ya mkewe. Mke alimuachia shilingi alfu tatu asubuhi. Sasa kama sio uchizi huu ni nini sasa? Asubuhi anaamka ana shilingi alfu tano anajifanya mtu mzuri anamwambia mkewe, ‘Tugawane hii we chukua alfu tatu mi nipe alfu mbili hali ngumu mke wangu’. Pambafu.
Halafu machizi wengine ni hawa wazazi ambao mzee mfanya kazi mshahara wake laki nne kwa mwezi, mkewe mama ntilie anauza maandazi, kila saa kumi alfajiri anakuwa tayari yuko mtaani anajaribu kukusanya shilingi alfu mbili tatu, wazazi hawa wakikusanya kipato chao kwa mwezi hakifiki laki saba. Wana binti yao yuko kidato cha pili, ana simu kali mbili, kila moja bei yake si chini ya laki nane. Wazazi wanaona poa tu, hawajui wapi kapata simu, wapi anapata vocha. Tena mara nyingine wanamuomba awapigie simu ndugu na jamaa, kama sio uchizi ni nini? Wacha nicheke barabarani peke yangu mie.

24 August 2017

USHAURI KWA WAPENZI WA ARSENAL

KIKUKWELI kwanza lazima niwape sifa wapenzi na mashabiki wa Arsenal. Hawa ndio wapenzi wa ukweli, sitaki kueleza kwanini lakini wenyewe wanajua.
Hawajali jua wala mvua roho yao kwa klabu yao. Lakini kuna kitu nimeona niongelee nacho ni hii jezi yao mpya (angalia pichani). Kiukweli hii jezi ina matatizo kidogo katika mchezo wa soka tunaoufahamu wengi, hivyo nashauri msitumie jezi hii kwenye mechi zenu kwa kuwa mtavuna magoli yasiyo idadi. Najua kufungwa hakutawafanya muhame timu lakini tukubaliane sio vizuri wakuu kama nyinyi tukisikia mmefungwa magori ishirini. Nadhani jezi hii inaweza kufanya vizuri kwenye timu yenu ya mchezo wa marede, lakini ni ushauri tu asante sana